Na Cresensia Kapinga, JamhuriMedia, Songea
Bodi ya Filamu na Michezo ya Kuigiza Tanzania (TFB) imeendesha mafunzo kwa wasanii 200 wa tasnia ya filamu wa manispaa hiyo ili kuwajengea uwezo wa kuzalisha filamu zenye ubora na zinazokidhi soko la ndani.
Mafunzo hayo yamefanyika Novemba 23, 2024 katika Manispaa ya Songea, ambapo baadae yalifungwa na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) aliyewasisitiza wasanii hao, kupitia mafunzo waliyopata wazalishe kazi bora ambazo zitafungua fursa mbalimbali za kiuchumi katika kazi zao.
“Sisi Wizara tumekuja na falsafa inayosema, Sanaa ni Ajira, Biashara na Uchumi, Takwimu zinasema watu zaidi ya 76,000 nchi nzima wamejiajiri katika sekta ya filamu hivyo tumieni mafunzo haya kutengeneza kazi bora ili kutengeneza ajira na uchumi” amesema Mhe. Ndumbaro
Waziri Ndumbaro amewaeleza wasanii hao juu ya fursa ya mikopo inayotolewa na Mfuko wa Utamaduni na Sanaa huku akiwasisitiza kujirasimisha ili waweze kunufaika na mfuko huo ili kuboresha kazi zao.
Kwa upande wake Katibu wa Chama cha Waigizaji Songea Bw. Shukrani Faraji ameishukuru Serikali kwa kutoa mafunzo hayo ambayo amekiri kuwa yataleta tija zaidi katika kazi zao huku akiomba mafunzo hayo yawe ya mara kwa mara.
Kwa upande wake afisa maendeleo ya Film kutoka bodi ya Film lakini pia mratibu wa mafunzo kwa wadau wa film na Michezo ya kuigiza nchini Alid Mpakata alisema kuwa bodi ya film inashughuli nyingi lakini shughuli moja wapo katika shughuli nyingi ni kwamba inahakikisha inatoa mafunzo kwa wadau wa watengeneza film upande wa uongozaji, uigizaji, upigaji picha na yanaenda mikoa tote Tanzania ikiwa sambamba na kuhamasisha wananchi upigaji jura serikali za mitaa.