Urusi ina akiba ya makombora mapya yenye nguvu “tayari kutumika”, Rais Vladimir Putin amesema, siku moja baada ya nchi yake kurusha kombora jipya la masafa marefu katika mji wa Dnipro nchini Ukraine.
Katika hotuba aliyoitoa katika runinga ambayo haijaratibiwa, kiongozi huyo wa Urusi alisema kuwa kombora la Oreshnik halikuweza kuzuiwa na kuahidi kufanya majaribio zaidi, ikiwa ni pamoja na “hali ya mapigano”.
Utumizi wa Urusi wa kombora la Oreshnik ulimaliza wiki moja ya kuongezeka kwa vita ambavyo pia vilishuhudia Ukraine ikirusha makombora ya Marekani na Uingereza hadi Urusi kwa mara ya kwanza.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alitoa wito kwa viongozi wa dunia kutoa “jibu zito” ili Putin “ahisi matokeo halisi ya matendo yake”.
Taifa lake lilikuwa likiwataka washirika wake wa Magharibi kuipatia nchi hiyo mifumo imara ya ulinzi wa anga, aliongeza.
Kulingana na shirika la habari la Interfax-Ukraine, Kyiv inatafuta kupata mfumo wa ulinzi wa Marekani wa (THAAD), au kuboresha mifumo yake ya ulinzi wa anga dhidi ya makombora ya masafa marefu.
Katika hotuba ya Ijumaa Putin alisema makombora ya Oreshnik hypersonic yaliruka mara 10 ya kasi ya sauti na kuamuru yaendelee kuzalishwa. Hapo awali alisema kuwa matumizi ya kombora hilo ni jibu kwa matumizi ya Ukraine ya makombora ya Storm Shadow na Atacms.
Shambulio la siku ya Alhamisi mjini Dnipro lilielezewa kuwa la kawaida na kwa mujibu wa walioshuhudia lilisababisha milipuko ambayo iliendelea kwa saa tatu.
Shambulio hilo lilikuwa na nguvu sana hali ambayo iliwafanya maafisa wa Ukraine kusema linafanana na kombora la masafa marefu (ICBM).
Justin Crump, Mkurugenzi Mtendaji na mwanzilishi wa kampuni ya ushauri wa hatari ya Sibylline, aliiambia BBC kwamba Moscow huenda ilitekeleza shambulio hilo kama onyo, akibainisha kuwa kombora hilo – ambalo ni la kasi na la kisasa zaidi ya mengine lina uwezo wa kukabiliana na Ukraine anga ya Ukraine.