Na Cresensia Kapinga, JamhuriMedia, Songea

Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea ambaye pia ni msimamizi wa uchaguzi katika Manispaa hiyo Bashir Muhoja amewashukuru waandishi wa habari kwa mchango wao mkubwa wa kupasha habari tangu kwa kuanza zoezi la uandikishaji na katika kuhakikisha kuwa upigaji kura unafanyika kwa ufanisi na kwa kuzingatia taratibu za uchaguzi.

Mshikamano na ushirikiano wa waandishi wa habari umeonekana kuwa na umuhimu mkubwa katika kutoa taarifa za haraka na za kuaminika kwa wananchi, hivyo kuhakikisha kuwa mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa unakuwa wazi  kwa umma.

“Mpaka sasa naweza nikasema kwanza niwashukuru sana ninyi waandishi wa Habari kwa msaada mkubwa mmetupa tangu tumeanza zoezi hili kupasha habari mbalimbali kwa hatua mbalimbali ikiwa ni hatua za uandikishaji ambapo mlitusaidia sana na kufanikiwa kwenye Mkoa wetu tuliongoza Manispaa kwa kuandikisha wananchi 186,000 ambayo kwa kweli ni idadi kubwa ikiwa ni asilimia 106 ya makadirio ambayo tulikuwa tumekadiria” amesema Muhoja.

Mkurugenzi wa Manispaa Bashir Muhoja akizungumza na waandishi wa Habari Jana ofisini kwake kuhusiana na uchaguzi wa serikali za mitaa.

Amesema kuwa wamebakiza siku tatu ambapo wananchi wa manispaa ya Songea watawachaguwa wenye viti wa mitaa 94 lakini  pia watawachaguwa wajumbe wale wa kundi mchanganyiko pamoja na kundi maalum la Wanawake ambapo amesema vyama zaidi ya saba vimejitokeza kuwa na wagombea jambo ambalo amesema sio dogo na kuendelea kuwa na utulivu.

Aidha, msimamizi huyo ameahidi kuendelea kushirikiana na vyombo vya habari ili kuhakikisha kuwa wananchi wanapata taarifa sahihi na za kutosha kuhusu uchaguzi na masuala mengine muhimu yanayohusu maendeleo ya Manispaa ya Songea.