Wagombea wanawake wa nafasi mbalimbali za uongozi katika Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara, kipindi hiki cha kampeni wametakiwa kujikita kunadi sera zinazowagusa zaidi wananchi, namna ya kuzitatua na kushughulikia kero za sehemu husika

Akizungumza wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wanawake hao kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024, Meya wa Manispaa hiyo Shadida Ndile amesema wanapokuwa kwenye kampeni wanadi sera zao na kuomba kura kwa wananchi wote bila kusemea chama kimoja pekee.

Amesema wanapogombea nafasi hizo ni vema wakatambua kuwa hawachaguliwi na chama kimoja pekee bali hata vyama vingine wanaweza kuwapigia kura kutokana na sera zao.

“Tunachohitaji ni kuona tunaongeza wanawake kwenye vyombo vya uamuzi na mwanamke ambae anaweza kuwa kiongozi anaweza kutoka kokote, kimsingi awe tu na ajenda ya kuwaletea wananchi maendeleo na unapokwenda kwenye uongozi huchaguliwi na chama chako pekee,”amesema Ndile.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilo la kiserikali linalojishughulisha na masuala mbalimbali ya kijamii mkoani Mtwara la Faidika Wote Pamoja (FAWOPA), Baltazar Komba amewataka wagombea hao kujipanga na kuhimili mapingamizi yanayotokana na harakati za kampeni ili waweze kufikia lengo husika.

“Tunaenda kwenye kampeni tumewaeleza wanawake kuwa wanaweza kukutana na mambo yake binafsi kwenye kampeni hivyo wanatakiwa kujiandaa kisaikolojia kupokea hayo maneno na kama wanawake mnatakiwa kuhakikisha mnajipanga kuweza kumudu hali hiyo,”amesema Komba

Mgombea wa nafasi ya uenyekiti katika Mtaa wa Mtepwezi Kata ya Likonde kwenye manispaa hiyo, Furaha Vitus kupitia Chama cha NCCR Mageuzi ameshukuru kitendo cha kupatiwa mafunzo hayo kwani yatamsadia kujiamini zaidi na kujua namna ya kukabiliana na changamoto zitazojitokeza kipindi hicho cha kampeni hadi kwenye uchaguzi huo.

Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Manispaa hiyo, Rida Kahungenge ambae pia ni Mratibu wa Mradi wa Wanawake, Uongozi na Haki za Kiuchumi unaofadhiliwa na Taasisi ya UNWOMEN amesema lengo la mafunzo ni kuwajengea uwezo wanawake hao ili waweze kusimama na kujiamini wakati wakiendelea na shughuli zao hizo.

Mafunzo hayo yameshirikisha wagombea hao 310 kutoka vyama mbalimbali vya siasa katika manispaa hiyo na kuandaliwa na Manispaa chini ya Mradi huo wa Wanawake, Uongozi na Haki za Kiuchumi unaofadhiliwa na Taasisi ya UNWOMEN.