Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
IMEELEZWA kuwa ili Tanzania iweze kukufikia azma ya kuwa kitovu cha madini barani Afrika ni lazima kujenga viwanda vitakavyoongeza thamani ya madini.
Hayo yameelezwa leo na Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mgeni Hassan Juma wakati akifunga Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini 2024 uliofanyika kwa siku tatu (Novemba 19-21, 2024) katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi.
Amesema uongezwaji wa Thamani katika madini ni jambo la muhimu, hivyo ni vyema kuhamasisha wadau kuwekeza katika kusaidia shughuli hiyo.
“Mijadala iliyofanyika kupitia Mkutano huu imejikita katika kutafuta suluhisho la changamoto zinazoikabili Sekta ya Madini, hususan katika nyanja za mitaji na teknolojia ya kisasa katika uongezaji thamani madini.
“Ili sekta iweze kuzalisha ajira zaidi na kuongeza mchango katika pato la taifa ni lazima madini yaongezwe thamani,” amesema.
Amebainisha kuwa, serikali imeweka mazingira rafiki kwa wawekezaji wa nje na ndani ambapo itasaidia kukuza sekta hiyo ya Madini nchini.
Kwa upande wake, Waziri wa Madini Anthony Mavunde amesisitiza kuwa, Mkutano huo umekuwa na mafanikio makubwa, kwani kwa mwaka 2024 umeleta washiriki zaidi ya 1500 kutoka Afrika na nje ya Africa kwa nia ya kubadilishana uzoefu.
“Kutokana na mahudhurio makubwa ya washiriki, tunafikiria kuwa na eneo letu maalum kwa ajili ya Mikutano ya Sekta ya Madini kama ilivyo kwa Mining Indaba kule Afrika Kusini, na ninawaomba Wakuu wa Mikoa kutenga maeneo maalum katika mikoa yao kwa ajili ya mikutano hii ya madini” amesema Mavunde.
Akizungumzia Kuhusu Sekta ya Madini visiwani Zanzibar, Mavunde alisema “Watu wakisikia Zanzibar wanachofikiria ni utalii, lakini miezi michache iliyopita Ripoti ya Utafiti wa Madini kule Zanzibar, Pemba yamegundulika madini tembo (Heavy Mineral Sands) hivyo kupitia rasilimali hiyo tunaamini uwekezaji mkubwa utafika pemba na tutaona manufaa ya uwepo wa rasilimali hizo na itasaidia kufungua uchumi wa Zanzibar“
Naye, Waziri wa Maji, Nishati na Madini Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Shaib Hassan Kaduara amesema kuwa, kama taifa moja ni muhimu kuimarisha ushirikiano katika eneo la utafiti wa kina wa madini kwa manufaa ya pande zote na kuongeza kuwa “Ni fahari kubwa kujua tuna rasilimali hizi na tunaahidi kuzisimamia kwa manufaa ya vizazi vilivyopo na vijavyo”
Awali akizungumza Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa amesema kuwa, Kaulimbiu ya Mkutano “Uongezaji Madini Thamani kwa Maendeleo ya Kiuchumi kwa Jamii” (Mineral Value Addition for Social – Economic Development) ikiwa na lengo la kuhamasisha shughuli za uongezaji thamani madini nchini kwa maendeleo ya Kiuchumi kwa Jamii.
Aidha, Dkt. Kiruswa amebaisha kuwa, Kaulimbiu hiyo inaenda sambamba na utekelezaji wa Sera ya Madini ya 2009 ambayo inaitaka Serikali kuhakikisha madini yanayozalishwa nchini yanaongezewa thamani kabla ya kusafirishwa kwenda nje ya nchi ili kupanua wigo wa mnyororo wa thamani kupitia fursa za ajira na uanzishwaji wa viwanda vya kuchakata madini nchini.
Mkutano wa mwaka huo wa Uwekezaji wa Katika Sekta ya Madini 2024 umedhihirisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha uwekezaji katika sekta ya madini, na umefungua njia kwa Zanzibar kushiriki kwa kina katika mpango wa maendeleo endelevu ya rasilimali madini.