Urusi inakadiriwa kuipatia Korea Kaskazini zaidi ya mapipa milioni moja ya mafuta tangu Machi mwaka huu, kulingana na uchambuzi wa picha za satelaiti kutoka kwa Open Source Centre, kikundi cha utafiti kisicho cha faida chenye makao yake makuu nchini Uingereza.

Mafuta hayo ni malipo ya silaha na wanajeshi Pyongyang wameituma Moscow kuendeleza vita vyake nchini Ukraine, wataalam wakuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, David Lammy, wameiambia BBC.

Uhamisho huu unakiuka vikwazo vya Umoja wa Mataifa, ambavyo vinapiga marufuku nchi kuuza mafuta kwa Korea Kaskazini, isipokuwa kwa kiwango kidogo, katika jaribio la kukandamiza uchumi wake ili kuizuia kuendeleza silaha za nyuklia.

Picha za satelaiti, zilizoshirikiwa pekee na BBC, zinaonyesha zaidi ya meli kumi na mbili tofauti za mafuta za Korea Kaskazini zikiwasili kwenye kituo cha mafuta Mashariki ya Mbali nchini Urusi jumla ya mara 43 katika kipindi cha miezi minane iliyopita.

Picha zaidi, zilizochukuliwa za meli hizo baharini, zinaonekana kuonyesha meli hizo zikiwasili zikiwa tupu, na kuondoka zikiwa zimekaribia kujaa.

Korea Kaskazini ndio nchi pekee duniani ambayo hairuhusiwi kununua mafuta kwenye soko la wazi. Idadi ya mapipa ya petroli iliyosafishwa inaweza kupokea inapunguzwa na Umoja wa Mataifa kuwa 500,000 kila mwaka , chini ya kiwango kinachohitajika.