Na Alex Kazenga, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa ameipongeza Wizara ya Madini pamoja na Sekta ya madini nchini kwa juhudi mbalimbali zinazofanyika kuiimarisha.

Pongezi hizo zimetolewa na Waziri Mkuu, Novemba 19, 2024 wakati akifungua mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini kwa mwaka 2024 unaoendelea katika Kituo cha Mikutano Cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

“Sekta ya madini imekua kwa asilimia 11.3 kwa sasa na mchango wake kwenye kuchangia pato la taifa umefikia asilimia 9.0,” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.

Ukuaji wa sekta hiyo amesema umechochewa na uwepo wa Sera nzuri zenye ushawishi, mazingira salama yenye utulivu na amani.

Sambamba na uwepo wa masoko ya uhakika yaliyounganishwa na jiografia nzuri ambavyo kwa pamoja vimechocheo kwa kiwango kikubwa ukuaji wa Sekta ya madini nchini.

“Serikali itaendelea kuboresha miundombinu yote inayohusiana na mnyororo mzima wa thamani ya madini, kwa kuboresha Barabara, nishati ya umeme na kuongeza idadi ya vituo vya mauzo na masoko ili kuiweka sekta kwenye ubora na ushindani,” amesema.

Kwa upande wake, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde akizungumza kwenye mkutano huo amesema Tanzania imeendelea kunufaika na rasilimali za madini kwa kuhakikisha serikali inapata mapato stahiki.

Manufaa hayo amesema yanatokana na Wizara ya Madini kuimarisha usimamizi wa shughuli za madini vizuri ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wananchi ndio wanakuwa wananufaika wakubwa.

Kuhusu mwenendo wa ukusanyaji mapato, Mavunde amesema kiwango cha ukusanyaji maduhuli ya Serikali kimepanda kutoka Sh bilioni 624.61 kwa mwaka 2021 hadi kufikia Sh bilioni 753.83 kwa mwaka 2023.

Amefafanua ukuaji wa Sekta ya Madini kwa mwaka 2021 kufikia asilimia 9.3 huku kwa mwaka 2023 ukuaji huo ukiongezeka hadi kufikia asilimia 11.3 huku mchango wake katika Pato la Taifa nao ukiongezeka kutoka asilimia 7.2 hadi 9.3.

Naye, Makamu Rais wa AngloGold Ashanti, Simon Shayo akizungumza kwenye mkutano huo, amesema Kampuni ya GGML, imeanza majadiliano na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ya kuiuzia dhahabu pamoja na Mpango wa kutumia viwanda vya ndani vya kusafisha dhahabu.

Shayo anayeshughulikia suala la Mahusiano na Maendeleo Endelevu (Afrika) katika kampuni hiyo amesema kwa sasa pia wameunganishwa kweye Gridi ya Taifa ya umeme.

“Kwa sasa tunatumia umeme wa uhakika ndani ya mgodi wetu (GGM), tofauti na huko nyuma tulipotumia nishati ya mafuta na kusababisha gharama za uendeshaji zilikuwa kubwa,” amesema Shayo.