Jeshi la Urusi linasonga mbele kwa mafanikio makubwa, katika mstari wa mbele wa vita nchini Ukraine, kwa mujibu wa utafiti.

Taarifa kutoka Taasisi ya Utafiti wa Vita (ISW) inaonyesha, kwa mwaka 2024 Urusi imenyakua karibu mara sita ya maeneo iliyonyakua mwaka 2023, na inasonga mbele kuelekea vituo muhimu vya ugavi vya Ukraine katika eneo la mashariki la Donbas.

Wakati huo huo, uvamizi wa kushtukiza wa Ukraine katika eneo la Kursk nchini Urusi unayumba. Wanajeshi wa Urusi wamewarudisha nyuma wanajeshi ya Kyiv.

Wataalamu wanatilia shaka mafanikio ya uvamizi huo wa Ukraine, huku mmoja akisema ni “janga la kimkakati” kutokana na uhaba wa wanajeshi wa Ukraine.

Mafanikio ya Urusi yanakuja wakati muhula wa pili wa Donald Trump unakaribia kuanza. Rais huyo mteule wa Marekani ameapa kumaliza vita hivyo atakapoingia madarakani mwezi Januari, huku wengine wakihofia huenda akapunguza msaada wa kijeshi kwa Ukraine.