Na Lookman Miraji, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Timu ya taifa ya waogeleaji imeanza safari leo Novemba 20 kuelekea nchini Burundi kushiriki mashindano Cana kanda ya tatu ya mwaka huu 2024( Cana zone 3 2024).

Kikosi hicho kimesafiri kikiwa tayari kushiriki mashindano hayo ya kimataifa yanayotarajiwa kuanza Novemba 22 na kuhitimika Novemba 24 jijini Bujumbura nchini humo.

Akizungumza katika hafla ya kuagwa kwa timu hiyo ya taifa Afisa michezo wa baraza la michezo la taifa BMT , Charles Maguzu amewaasa waogeleaji kuwa watumie sehemu ya mashindano hayo kuliheshimisha huku pia ikishuhudiwa mwaka huu kuwa ni mara ya kwanza kwa Tanzania inapeleka timu ya waogeleaji kutoka katika daraja la juu zaidi(masters category).

“Imani iliyopo kwenu ni kubwa sana kuanzia kwa makocha wenu mpaka kwetu sisi viongozi hivyo tutategemea kuona mnarudi na medali za kutosha. Hakikisheni mnashindana kwa mioyo mmoja huku mkiwa na kumbukumbu kuwa mnalipambania taifa kama wapiganaji ili kulinda heshima ya taifa letu”

Aidha Afisa Maguzu pia ametoa pia shukrani za dhati kwa kampuni ya Great lake zone kwa kugharamia gharama za timu hiyo kuelekea nchini Burundi huku akisema hatua hiyo ni namna mojawapo ya kuiunga mkono serikali katika jitihada zake za kuinua michezo nchini.

Kwa upande pia mwalimu wa timu hiyo ya waogeleaji Michael Livingstone nae amesema kuwa anaamini katika maandalizi ya kikosi hicho kwani wamekuwa wakijifua kwa muda mrefu kwaajili ya mashindano hayo ambayo anaamini kuwa ushiriki wao utaliheshimisha taifa.

Aidha nae nahodha wa timu hiyo ya waogeleaji Colins Saliboko ameahidi kuwa watarejea na ushindi huku akionyesha kuridhishwa na maandalizi waliyoyapata kutoka kwa benchi la ufundi.

Kikosi hicho kimesafiri kikiwa jumla ya waogeleaji 38 pamoja viongozi wa chama wakiongozwa na mwenyekiti wa chama cha kuogelea (TSA) , David Mwasyoge.