Katika uchaguzi mkuu wa urais uliofanyika Novemba 13 nchini Somaliland, kiongozi wa upinzani Abdirahman Mohamed Abdullahi, maarufu kama “Irro”, ameibuka mshindi baada ya kupata asilimia 63.92 ya kura zote. Karibia watu milioni 1.2 walijitokeza kupiga kura, na zoezi hilo lilielezewa na waangalizi wa kimataifa kama la amani na la kuzingatia misingi ya demokrasia.

Rais anayeondoka madarakani, Muse Bihi, alipata asilimia 34.81 ya kura, huku kiongozi wa chama cha Social Justice Party (UCID), Faysal Ali Warabe, akipata asilimia 0.74.

Irro, ambaye ni balozi wa zamani wa Somalia katika muungano wa kisovieti na Finland, ameahidi kuleta mageuzi makubwa na kuwaunganisha raia wa Somaliland ambao wanajiona kama wamegawanyika chini ya utawala wa Rais Bihi. Alimtuhumu mtangulizi wake kwa kuchochea mapigano ya kijamii na kupoteza sehemu ya eneo la Sool katika vita dhidi ya wapiganaji wa Mogadishu.