Jimbo kuu la Kanisa Katoliki Nairobi limesisitiza kujitolea kwake kuzingatia sera ya Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini Kenya (KCCB) kuhusu michango ya kisiasa kanisani.

Hapo juzi, Jimbo Kuu lilitangaza kukataliwa kwa michango kadhaa iliyotolewa katika Kanisa Katoliki la Soweto, kwa mujibu wa maagizo ya KCCB na Muswada wa kuchangisha Fedha za Umma wa 2024.

Rais William Ruto alichangia shilingi milioni mbili ($15,504) kwa ujenzi wa nyumba ya Padri na kutoa ahadi ya shilingi milioni tatu kwa ajili ya ujenzi wa ziada na mchango wa mabasi ya parokia.

KCCB, katika taarifa yake iliyotolewa tarehe 14 Novemba, 2024 na kusomwa katika makanisa yote ndani ya Jimbo Kuu Jumapili, Novemba 17, 2024, ilisisitiza umuhimu wa kuhifadhi uhuru na utakatifu wa Kanisa, pamoja na masuala ya kimaadili yanayozunguka michango ya kisiasa.

Akizungumza kwa niaba ya Jimbo kuu Askofu mkuu Philip A. Anyolo, alisisitiza umuhimu wa majukwaa ya Kanisa kutotumiwa kujinufaisha kisiasa.