Katika tukio la kushangaza, mlima mmoja katika mkoa wa Katanga, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DR Congo) umesambaratika na kufichua akiba kubwa ya shaba.

Video inayonyesha tukio hilo imeenea kwenye majukwaa mbalimbali ya mitandao ya kijamii, ikionyesha umati mkubwa wa watu waliokuwepo eneo hilo wakati mlima ukisambaratika, huku baadhi yao wakikimbia kujiokoa.

Mkoa wa Katanga, DR Congo, unajulikana kwa utajiri wake mkubwa wa madini. Eneo hili liko ndani ya ukanda wa shaba wa Afrika, ukanda wa kilomita 450 unaotoka Luanshya kaskazini-magharibi mwa Zambia hadi Katanga, Congo.

Kwa zaidi ya karne moja, mkoa huu umekuwa kitovu kikubwa cha uchimbaji wa shaba. Katika miaka ya 1950, ulikuwa mzalishaji mkubwa zaidi wa shaba duniani.

Kwa sasa, mkoa huo unachangia zaidi ya asilimia kumi ya akiba ya shaba duniani, madini ambayo hupatikana hasa kutoka kwenye mashapo ya enzi ya Precambrian.

Akiba hii ya shaba ni mchango mkubwa kwa uchumi wa Zambia na Congo, ikichochea maendeleo ya miundombinu na kutoa fursa za ajira katika eneo hilo.

Shaba na kobalti zinachimbwa zaidi kwa ajili ya utengenezaji wa betri, hasa wakati huu ambapo dunia inahamia kwenye nishati safi. Mahitaji ya teknolojia za nishati safi yameongeza pia mahitaji ya metali kama shaba na kobalti.

Metali hizi ni muhimu kwa utengenezaji wa betri za lithiamu-ioni zinazotumika kwenye magari ya umeme.