Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Zanzibar
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Al hajj Dk. Hussein Ali Mwinyi, amewaongoza wafanyakazi wa Shirika la Utangazaji Zanzibar, (ZBC) familia na waumini wengine wa dini ya Kiislam kwenye maziko ya aliyekuwa Mwandishi wa habari wa Shirika hilo, marehemu, Biubwa Said Mbarak aliefariki dunia usiku wa kuamkia leo hospitali ya Taifa ya Muhimbili wakati akitibiwa.
Maziko hayo yamefanyika nyumbani kwao Marehemu Kwaalamsha, Wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi na baadae Al hajj Dk. Mwinyi alihudhuria sala ya maiti iliyohudhuriwa pia na wananchi mbalimbali.
Marehemu Biubwa kitaaluma alikua mwandishi wa habari, alipata mafunzo ya kada hiyo kwenye Chuo Cha Idara ya Habari Maelezo wakati huo mwaka 1999 na aliajiriwa na ZBC mwaka 2007, ambapo awali alikuwa mwandishi wa habari za mawio, kipindi maarufu kinachorishwa Kila siku asubuhi na ZBC, redio, akiwa miongoni mwa watangazaji wa mwanzo wa kipindi hicho tokea kilipoanzishwa mwaka 2000.
Baadhi ya waandishi wa habari waandamizi, na wafanyakazi wa ZBC, wameelezea namna walivyomfahamu marehemu Biubwa katika kazi zao, kwamba alikua mchapakazi, mweledi na mwenye ushirikiano mzuri na wenziwe na kwamba ameacha pengo kwenye tasnia ya habari.
Marehemu Biubwa alizaliwa mwaka 1972 na amezikwa kijijini kwao Jumbi, Mkoa wa Kusini Unguja.
Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahala pema peponi amin.