Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema kuwa angetamani vita na Urusi vimalizike mwaka ujao kwa njia za kidiplomasia, hasa wakati nchi zote mbili zikijiandaa kwa Donald Trump kurejea Ikulu.
Matarajio ya Trump kurejea madarakani yameibua maswali kuhusu hatma ya mzozo huo, kutokana na Mrepublican huyo kukosoa waziwazi msaada wa kijeshi kwa Kyiv.
Zelensky alizungumzia umuhimu wa diplomasia huku akikataa masharti ya Rais wa Urusi Vladimir Putin ya kuitaka Kyiv kuachia maeneo yalitwaliwa na Urusi.
Wakati huo huo, Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz alifanya mazungumzo ya simu na Putin, licha ya pingamizi kutoka Ukraine, ambayo iliiona hatua hiyo kama jaribio la kumfurahisha Putin.
Wakati mzozo ukiendelea, Zelensky amesisitiza hasara kubwa zinazovikabili vikosi vya Urusi, huku mataifa ya G7 yakirudia msimamo wake wa kuiunga mkono Ukraine, na kuilaumu Urusi kama kikwazo pekee cha amani.