Na Allan Kitwe, JamhuriMedia,Tabora
JESHI la Polisi Mkoani Tabora linawashikiria watu watatu kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya mwanamke aitwaye Sagali Masanja (62) bibi mkazi wa Kijiji cha Mahene Wilaya ya Nzega, kumkata titi na sehemu za siri na kuondoka nazo.
Kamanda wa Polisi Mkoani hapa SACP Richard Abwao amethibitisha kutokea tukio hilo alipokuwa akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake jana ambapo alieleza kuwa chanzo cha mauaji hayo ni imani za kishirikina.
Alisema kuwa tukio hilo limetokea Novemba 14 mwaka huu majira ya saa 7 usiku ambapo watuhumiwa walifanya mauaji ya bibi huyo kwa tuhuma kuwa ni mchawi na alihusika kumroga mtoto aliyefia kisimani.
Kamanda Abwao alibainisha kuwa marehemu aliuawa kwa kukatwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake na wauaji kuondoka na titi 1 na sehemu zake za siri, pia walichukua vitu mbalimbali ikiwemo begi lake la nguo.
Alifafanua kuwa baada ya kupata taarifa hizo kutoka kwa wananchi walifika eneo la tukio na kufanya msako mkali uliowezesha kukamatwa watuhumiwa hao watatu ambao ndio waliotuma wauaji kwenda kufanya tukio hilo.
Waliokamatwa ni Lucia Mabula (36) msukuma, mkazi wa Kijiji cha Mahene ambaye ndiye aliyetafuta wauaji na kuwalipa sh laki 2 ili wakamuue bibi huyo kwa madai kuwa alimroga mtoto wake mwaka 2023 na kufia kisima.
Wa pili ni Makenzi Mabula (49) ambaye ni mume wa Lucia Mabula, msukuma na mkazi wa Kijiji cha Mahene na wa 3 ni Ramadhani Kurwa (38) msukuma mkazi wa Mahene pia.
Kamanda Abwao alifafanua kuwa baada ya mauaji hayo kutokea usiku huo wananchi waliwakimbiza wauaji na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa 2 na mganga wa kienyeji aliyekuwa akiwapaka dawa ili wasikamatwe.
Waliokamatwa na wananchi usiku huo kwa mauaji hayo ni Masumbuko Ngassa (33) msukuma mkazi wa Kijiji cha Segese Wilaya ya Kahama Mkoani Sinyanga na Shilinde Kaseko (30) mkazi wa Kijiji cha Seki Wilayani Nzega.
Wa 3 ni Sana Maganga (66) msukuma, huyu alikuwa mganga wa kienyeji mkazi wa Kijiji cha Seki Wilayani Nzega ambaye ni mama mzazi wa Shilinde Kaseko.
Aliongeza kuwa baada ya kukamatwa wauaji hao, wananchi wenye hasira walijichukulia sheria mkononi na kuwapa kipigo kikali kisha kuwachoma moto ambapo watuhumiwa wote walipoteza maisha.
Alibainisha kuwa watuhumiwa hao baada ya kukamatwa walikutwa na titi 1 la binadamu, sehemu za siri na vitu walivyokuwa wameiba likiwemo begi la nguo za marehemu.
Kamanda Abwao alitoa wito kwa wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi na kuwataka kuachana na imani za kishirikina kwa kuwa ni imani potofu na zinaongeza fitina, chuki na uhasama pia zinasababisha madhara kwa jamii.