Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

IDADI ya watu waliopoteza maisha baada ya kufukiwa na jengo lililoporomoka Kariakoo jijini Dar es Salaam imefikia watano huku majeruhi waliookolewa wakiongezeka na kufikia 42.

Jengo hilo linaelezwa kuporomoka mapema leo Jumamosi Novemba 16, 2024 ambapo kwa mujibu wa mashuhuda wanaeleza kuwa kulikuwa na watu kadhaa waliokuwa wakifanya ununuzi katika maduka ya jengo hilo.

Mratibu wa matukio kutoka Jeshi la Zimamoto, Peter Mtui amethibitisha idadi hiyo ambapo amesema zoezi la uokoaji linaendelea.

Amesema juhudi za uokoaji mpaka sasa zinafanyika kwa njia ya mikono hadi saa 72 zipite ndipo vyombo vingine vya uokoaji vitaendelea.

Akizungumza baada ya kuwasili katika eneo hilo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema jitihada zinaendelea kwa kupeleka oksijeni nyingi zaidi na ya kutosha kwa waathirika wa jengo hilo.

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametoa pole kutokana na ajali hiyo, huku akiagiza nguvu ya uokoaji iongezwe ili kunusuru maisha ya waathirika wa ajali hiyo