Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi ndugu Khamis Jaaphar Katimba amewajengea uwezo wa kiutendaji Maafisa maendele ya Jamii wa Kata, Watendaji wa Vijiji na Watendaji Kata ili waweze ksimamia na kutekeleza vizuri majukumu yao.
Watendaji hao wamefahamishwa majukumu yao ambayo wanatakiwa kuyasimamia kikamilifu ikiwa ni pamoja na ukusanyaji wa mapato, usimamizi wa miradi na kuendeleza utawala bora.
Kwa upande wa mapato Watendaji hao wametakiwa kuwa na orodha ya vyanzo vyote vya ukusanyaji wa mapato vilivyo katika maeneo yao ikiwa ni pamoja na kuwa na orodha ya wamiliki wote wa biashara katika maeneo yao,na kuhakikisha kuwa katika kipindi hiki cha Mwezi Novemba wanawafikia Wafanyabiashara wote na kuwahamasisha kulipia leseni zao za biashara, na wasio na leseni wakate leseni na kuongeza kuwa Disemba mwanzoni kitafanyika kikao cha tathimini ya utekelezaji wa maelekezo hayo.
Kuhusu miradi Watendaji hao wameelekezwa kuwa wao ndiyo wasimamizi wakuu wa miradi hiyo hivyo ni wajibu wao kuhakikisha kuwa fedha zote zinazoenda katika utekelezaji wa miradi zinafanya kazi iloyokusuidiwa, wawe karibu na miradi hiyo na inapotokea changamoto watafute namna ya kutatua changamoto hizo badala ya kukaa kimya.
Ameelekeza ufanyikaji wa vikao vya menejimenti za Kata ambapo Maafisa maendeleo ya Jamii watakua Waratibu, na kuwa miradi ispotekelezwa kwa wakati wao ndio watakaowajibika , Maafisa hawa watahusika na shughuli zote ambazo zinaendelea katika Kata na Vijiji.
Katimba amesema kuwa Maafisa Maendeleo ya Jamii wamekumbushwa pia kuwa wao ndio kiungo kikubwa katika maendeleo ya Kata zao, lakini uzoefu unaonyesha kuwa wanajikita sana kwenye masuala ya mikopo na kusahau majukumu yao mengine.
Aliwaelekeza kuwa ni lazima washirikiane na Wataalam wengine wa Kata kuhakikisha wanabadilisha mitazamo hasi iliyopo katika Jamii na kuielekeza jamii katika mwelekeo unaohitajika.
“Katika maeneo yetu kuna baadhi ya watu ambao wana mitazamo tofauti kuhusu shughuli za maendeleo, kuna Watu ambao wanaamini mila na desturi hatarishi katika Jamii hivyo ni jukumu lenu kubadili mitazamo hii katika Jamii” alisema Katimba.
Akifunga mafunzo hayo Katibu Tawala wa Wilaya ya Malinyi Bi Saida Mhanga aliwataka Watendaji hao kutimiza wajibu wao hasa katika utawala bora , wakae ofisini kusikiliza na kutatua kero za Wananchi.
“Kumekua na malalamiko mengi yanatoka kwa Wananchi yanapelekwa kwa ofisi ya Mkuu wa Wilaya ambapo ukichunguza kwa makini unaona kwamba ni kutotekeleza majukumu ya Watendaji katika maeneo yao ambapo masuala haya yangeweza kutatuliwa katika maeneo yao”alisema Bi Saida Mhanga
Aidha amewataka Watendaji hao kuandaa box la kupokea maoni/mapendekezo kutoka kwa Wananchi, na kuongeza kuwa Watendaji hao waendeshe vikao vya kisheria na wasome taarifa za mapato na matumizi ili Wananchi wawe na Imani na Serikali yao.
Akitoa mada ya kuzuia na kupambana na rushwa Kamanda wa TAKUKRU Wilaya ya Malinyi Bi Sikujua Kimweri aliwataka Watumishi kuzingatia miongozo na taratibu za kazi.
Kamanda huyo alisema kuwa TAKUKURU ina lengo la kuhakikisha kuwa shughuli zote za Serikali zinapangwa na kufanyika kwa mujibu wa taratibu ili Wananchi waone kazi zinazofanywa na Serikali yao.
Bi Sikujua Kimweri aliwataka Watendaji hao kuhakikisha kuwa mapato ya Halmashauri yanakusanywa na yanatumika kwa usahihi kulingana na bajeti ilivyo.
Aliwataka Watendaji hao kuwa makini na fedha za miradi ambazo zinaenda kutekeleza miradi katika maeneo yao na kuongeza kuwa miradi hiyo itekelezwe kwa mujibu wa BOQ miongozo na kanuni za Serkali .
Amewataka Watendaji hao kuzingatia taratibu hizo kwasababu wakienda kinyume na taratibu hizo ndipo watakutana na mkono wa sharia, amewataka Watumishi kufanya kazi kwa weledi na kujiepusha na vitendo vya rushwa.
Kwa upande kilimo, mifugo na uvuvi , Mkuu wa Idara hiyo ndugu Gipson Absalom amewaambia Watendaji kuwa Idara yake inafanya kazi kwa ukaribu na mamlaka ya hali ya hewa na kwa mujibu wa utabiri wa hali ya hewa , Wilaya ya Malinyi itakua na mvua chache, za wastani na chini ya wastani, hivyo amewataka Watendaji washirikiane na maafisa kilimo waliopo katika Kata na VIjiji kutoa elimu kwa Wananchi kuhakikisha kuwa wanapanda mazao yanayostahimili maji au mvua chache na wale wanaotaka kulima mpunga wachague maeneo amabayo yana majimaji.