Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imesema kuwa inaendelea kuchukua hatua mbalimbali katika Kudhibiti athari za Huduma za mikopo ya kidigitali ikiwemo kuelimisha umma kutumia Huduma ndogo za Fedha zinazotolewa na mtoa Huduma mwenye leseni ya Benki Kuu.
Aidha imesema kuwa hadi kufikia Novemba 14, mwaka huu maombi 20 yaliyopokelewa na wametoa vibali vinne kwa Taasisi nne.
Hayo yameelezwa na Meneja Msaidizi Idara Ndogo za Fedha kutoka BoT, Marry Ngasa, wakati wa mafunzo kwa wahariri na waandishi wa habari kuhusu usimamizi wa mikopo ya mitandaoni.
“Tunaendelea kutoa elimu na taratibu za ukusanyaji madeni ambazo zinakataza waziwazi vitendo vya lugha za matusi, vitisho na kukaripia.
“Vilevile tumeweka dawati la malalamiko Benki Kuu, Kushirikiana na TCRA ili kuzifunga Apps 55 zilizogundulika kutoa Mikopo mitandaoni bila kuwa na kibali cha Benki Kuu na kuhakikisha kunakuwa na uwazi katika riba na gharama,” amesema.
Amebainisha kuwa, watoa mikopo wanatakiwa kufafanua kwa uwazi wa viwango vya riba na ada zote kwa wateja kabla ya kutoa Mikopo.
Ameongeza kuwa, pia wanahakikisha kunakuwa na Ulinzi wa taarifa za wateja na Benki Kuu imeweka takwa la kulinda taarifa binafsi za wateja ili kuepuka upotevu au matumizi mabaya ya taarifa hizo kama ilivyoainishwa kwenye Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ya mwaka.
Awali akifungua mafunzo hayo, Kaimu Meneja Huduma Ndogo za Fedha, Dickson Gama amesema ni jukumu la BoT kusimamia taasisi za fedha hivyo itaendelea kuhakikisha sekta ya fedha inakuwa thabiti, imara na stahimilivu.
Amesema Benki Kuu imeandaa semina hiyo kwa wahariri na waandishi wa habari lengo ni kwajengea uelewa ili waweze kuelimisha umma.
“Ni jukumu la BoT katika kusimamia huduma Ndogo za fedha nchini hivyo kwa kutambua umuhimu wa vyombo vya habari kama kiunganishi kati ya Benki Kuu na jamii ya watanzania na dunia kwa ujumla tunaamini kupitia mafunzo haya mtaenda kuelimisha umma na kujiepusha na mikopo ya kitapeli,” amesema Gama.
Ameongeza kuwa semina hiyo ina umuhimu mkubwa kutokana na ongezeko la huduma za utoaji mikopo mitandaoni pamoja na changamoto zake.
Ameeleza kuwa mikopo ya mitandaoni imekuwa ni sehemu ya mfumo wa fedha kwani imerahisisha utoaji wa huduma za mikopo kwa urahisi zaidi na haraka.
Amesema ukuaji huo wa haraka umesababisha changamoto kadhaa ikiwemo masuala ya kimaadili, riba kubwa gharama kubwa za mikopo na kukosekana kwa taarifa.
Gama amesema kutokana na changamoto hizo wamekuwa mstari wa mbele kutoa elimu ili kufanya huduma hiyo kuwa na manufaa kwa wananchi na mtoa huduma kuidhinishwa na BoT.
Amewataka watanzania kukopa kwa maendeleo lakini pia kuchukua hatua pindi taarifa zao zinapodukuliwa bila ridhaa zao kitendo kinachofanywa na wakopeshaji.