Serikali kupitia Wizara ya Afya haitasita wala kusitisha ushirikiano uliopo baina ya ubalozi wa India pamoja na Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa nchini Tanzania (USAID) ili kuendelea kuboresha Sekta ya Afya nchini.
Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema hayo Novemba 14, 2024 baada ya kukutana na Mkurugenzi wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa nchini Tanzania (USAID) Dkt. Craig Hart pamoja na Balozi wa India nchini Tanzania Mhe. Bishwadip Dey katika ofisi ndogo za Wizara ya Afya jijini Dar es Salaam.
Katika kikao hicho Waziri Mhagama amesema kwa upande wa USAID wamekua wakisaidia Sekta ya Afya nchini hasa katika uboreshaji wa huduma za VVU/UKIMWI, Malaria, Lishe, Kifua Kikuu, uzazi wa mpango, afya ya uzazi, mama na mtoto.
“Vilevile, Ubalozi wa India nchini Tanzania wamekua wakishirikiana na Tanzania katika Sekta ya Afya kwenye maeneo ya mafunzo ya wataalamu wa afya, kubadilishana kwa wataalamu wa afya kutoka nchi moja kwenda nyingine pamoja na rufaa za wagonjwa na ushauri wa matibabu mtandaoni,” amesema Waziri Mhagama
Aidha, Waziri Mhagama amesema Ubalozi wa India nchini Tanzania uliingia makubaliano ya mkataba pamoja na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya na ‘Hester Biosciences Ltd (India) tarehe 09 Oktoba, 2023 kwa madhumuni ya kuanzisha kiwanda cha kutengeneza dawa za binadamu na mifugo nchini.
Waziri Mhagama ameomba ushirikiano kutoka kwa USAID katika kupunguza vifo vya mama na mtoto pamoja na vifo vya watoto wachanga ambapo kwa sasa vifo vya watoto wachanga vimepungua kutoka vifo 25 kwa kila vizazi hai 1,000 mwaka 2015/16 hadi 24 kwa kila vizazi hai 1,000 mwaka 2021/2022.
“Lakini pia natoa rai kwa USAID pamoja na ubalozi wa India nchini Tanzania kusaidia wahudumu wa afya ngazi ya jamii ambao wanatoa elimu na uhamasishaji wa upimaji wa magonjwa mbalimbali pamoja na kusaidia mzigo mkubwa wa magonjwa yasiyoambukiza ambayo yamekuwa yakiongezeka kila mwaka nchini,” amesema Waziri Mhagama
Mwaisho, Waziri Mhagama amewashukuru wadau hao kwa kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuboresha huduma za afya ambapo amewaahidi kuendeleza ushirikiano huo na kuwaunga mkono katika utendaji kazi wao.