Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mtwara
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mhandisi Victor Seff amewataka Wahandisi wa TARURA nchini kutoa ushauri wa kitaalamu kwa wananchi na wadau wa maendeleo pindi wanapofungua au kutengeneza barabara kwa nguvu zao kwa barabara ambazo hazipo kwenye mtandao unaosimamiwa na TARURA.
Mhandisi Seff ameyasema hayo wakati akiongea na watumishi wa TARURA Mkoni Mtwara katika ziara yake ya kikazi ya ufuatiliaji wa miradi ya ujenzi na matengenezo ya miundombinu ya barabara.
Amesema wadau hao wanaojitolea kufungua barabara katika maeneo yao lengo lao ni zuri, hivyo wanahitaji ushauri wa kitaalamu ili kuweza kutengeneza barabara zitakazodumu kwa muda mrefu.
Naye Meneja wa TARURA Wilaya ya Nanyamba Mhandisi Hussein Mwombeki amemweleza Mtendaji Mkuu kuwa Wilaya hiyo ina ongezeko la barabara ambazo hazipo kwenye Mtandao wa barabara za TARURA zilizofunguliwa na vikundi vilivyo kwenye Mradi wa TASAF.
Hata hivyo, Mhandisi Seff ametumia fursa hiyo kuwapongeza watumishi wa TARURA Mkoa wa Mtwara na Wilaya zake kwa kazi nzuri zilizoiletea sifa TARURA.
Aidha, Mtendaji Mkuu huyo amewaasa watumishi kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kutoharibu sifa zinazopokelewa na Wakala.
Katika ziara hiyo Mhandisi Seff ametembelea Ofisi za TARURA wilaya ya Masasi, Nanyumbu, Tandahimba, Nanyamba pamoja na kukagua miradi ya ujenzi wa barabara zilizoathirika na mafuriko ya mvua msimu uliopita.
Baada ya kumaliza ziara yake Mkoani Mtwara, Mhandisi Seff anaelekea Mkoani Lindi kufanya ufuatiaji wa kazi zinazofanywa na TARURA pamoja na kuongea na Watumishi Mkoani humo.