Na Allan Kitwe, JamhuriMedia, Tabora

Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imepeleka kiasi cha sh bil 19 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa usambazaji nishati ya umeme vijijini (REA) katika vitongoji 180 vya Mkoa wa Tabora.

Hayo yameelezwa juzi na Msimamizi wa Miradi ya REA Kanda ya Magharibi, Mhandisi Robert Dulle katika hafla ya kumtambulisha Mkandarasi aliyeshinda zabuni ya kutekeleza mradi huo Kampuni ya Sinotec Company Ltd ya China.

Ameeleza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan ameridhia kiasi hicho kitumike kufikisha huduma ya umeme katika vitongoji vyote 180 hivyo kunufaisha kaya zaidi ya 5,900.

Mhandisi Dulle amefafanua kuwa mradi huo utatekelezwa katika majimbo yote 12 ya Mkoa huo kwa muda wa miaka 2 na matarajio yao ni kukamilisha kazi hiyo kabla ya mwezi Agosti 2026 ambapo vitongoji 15 katika kila jimbo vitanufaika.

Amebainisha kuwa hadi sasa vitongoji 1,323 vimeshafikishiwa huduma hiyo na vitongoji 3,749 vilivyobakia kazi inaendelea na kuongeza kuwa vitakavyobakia vitaendelea kusambaziwa huduma hiyo kadri fedha zitakavyopatikana.

Ametaja Majimbo yatakavyonufaika kuwa ni Sikonge, Urambo, Igalula, Tabora Kaskazini, Kaliua, Ulyankulu, Bukene, Nzega Vijijini, Nzega Mjini, Igunga, Tabora Mjini na Manonga ambapo kila jimbo vitongoji 15 vitapata huduma hiyo.

Mhandisi Dulle amesisitiza kuwa gharama ya kuunganishiwa umeme kwa wananchi ndani ya vitongoji hivyo ni sh 27,000 tu huku akitahadharisha kuwa mradi hautakuwa na fidia kokote utakapopita.

Amefafanua kuwa Wakala kwa kushirikiana na Shirika la Umeme (TANESCO) wanaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya umeme nchi nzima na kusimamia ipasavyo wakandarasi wote waliopewa zabuni ya kutekeleza miradi hiyo.

Akiongea katika hafla hiyo Mkuu wa Mkoa huo Paul Matiko Chacha alimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuwaletea kiasi hicho cha fedha na kumhakikishia kuwa watasimamia ipasavyo mradi huo ili ukamilike kwa wakati.

Amemwagiza Mkandarasi kufanya kazi hiyo usiku na mchana ili kuhakikisha umeme huo unafikishwa katika maeneo yote yaliyoainishwa kwenye mkataba kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.

RC ameeleza kuwa ujio wa mradi huo ni hatua muhimu sana kwa wananchi kwa kuwa utasaidia kuchochea kasi ya maendeleo yao kwa kuongeza thamani ya mazao, ufundi seremala, viwanda vidogo vidogo, mashine za kusaga na kukoboa sambamba na shughuli nyingine za kiuchumi na kijamii.

Naye Meneja wa Mradi kutoka Kampuni ya Sinotec Company Ltd, Mhandisi Alphred Kessy amemuhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa watakamilisha mradi kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.