Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

SHIRIKA la Taifa la Bima (NIC) imezindua msimu wa pili wa Kampeni ya ‘NIC KITAA’ yenye lengo la kutoa elimu ya Bima kwa watanzania ili waelewe faida na muhimu wake.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa NIC, Kaimu Mkeyenge amesema kuwa asilimia mbili ya Watanzania wana uelewa kuhusu elimu ya bima huku lengo ni kufikia asilimia tano.

Amesema wanaingia msimu wa pili wa kampeni wa NIC Kitaa kusogeza huduma kwa wananchi na kuhakikisha elimu ya bima inawafikia wote na kutambua umuhimu wa bima.

“Pamoja na kutoa elimu ya kampeni hii pia tatambatisha na kuandikisha bima kwa wateja wapya. Na wale wanaolipa madeni sio lazima waje ofisini tumewasogezea huduma mitaani,” amesema.

Ameeleza kuwa kampeni hiyo itafanyika nchi nzima kwa sasa wameanza na mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma na Singida.

“Kutoa elimu hii ni kuendeleza sera ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya bima kwa wote na kuhakikisha watanzania wote wanatumia bima.

“Na Sisi kama Taasisi kongwe ya serikali tunawajibu wa kuisaidia serikali ili wawe na uelewa wa kutosha wa kuhusu umuhimu wa kukata bima,” amesisisitiza.