Na Alex Kazenga, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imemnasa kinara wa kusambaza dawa za kulevya jijini Dodoma; JAMHURI linaripoti.
Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo akizungumza na vyombo vya habari Novemba 12, 2024 jijini Dar es Salaam amesema wamemkamata Suleiman Mbaruku maarufu Nyanda ambaye wamekuwa wakimtafuta kwa muda mrefu.
Mbaruku mwenye umri wa miaka 52 amekamatwa akiwa na mwenzake, Kimwaga Lazaro mwenye umri wa miaka 37 wote wakazi wa mtaa wa Kinyeli kata ya Viwandani jijini humo.
“Huyu Nyanda ni maarufu sana jijini Dodoma, waraibu tunaowatibu katika kituo cha pale Dodoma wengi wao wameharibiwa na Nyanda,” amesema Kamishna Jenerali Lyimo huku akisisitiza kuwa mamlaka imekuwa ikimfuatilia kwa muda mrefu.
Amesema Nyanda na mwenzake walikutwa na jumla ua gramu 392 za dawa za kulevya aina ya Heroin na kwamba hatua za kisheria dhidi yao zinaendelea.
Kamishna Jenerali Lyimo amesema wamefanikiwa kukamata vinara hao katika operesheni waliyoiendesha nchini kati ya Oktoba na Novemba 2024 ambapo jumla ya kilo 1,066.105 za dawa za kulevya zimekamatwa.
Ukamataji huo ulienda sambamba na kukamatwa kwa mililita 447 za dawa tiba zenye asili ya kulevya, uteketezwaji wa ekari 157.4 za mashamba ya bangi, lita 19,804 za kemikali bashirifu pamoja na watuhumiwa 58.
Kati ya dawa hizo amesema walikamata kilogramu 687.32 ya skanka na kilo moja ya hashishi katika eneo la Goba, jijini Dar es Salaamzikiwa zimefichwa ndani ya nyumba za watuhumiwa.
“Uchunguzi wetu umebaini wateja wengi wa skank ani wanawake, hudai kutumia dawa hizo kunawapunguzia msongo wa mawazo na kujistarehesha.
“Skanka ni aina ya bangi yenye kiwango kikubwa cha sumu, inayosababisha madhara makubwa kiafya, vile vile hashish ambayo hutengenezwa kwa mchanganyiko wa maua na mafuta ya mbegu za bangi inapovutwa huzalisha kemikali hatari zinazoweza kusababisha magonjwa ya akili kwa haraka,” amesema Kamishna Jenerali Lyimo.
Aidha, amesema katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, DCEA ilikamata mililita 120 za dawa tiba zenye asili ya kulevya aina ya Codein zikiwa zinasafirishwa kwenda nje ya nchi.
Sambamba na ukamataji wa mililita 327 za dawa hizo zilizokutwa nyumbani kwa mtuhumiwa eneo la Tabata Kinyerezi.
Dawa hizo ziliingizwa nchini kinyume cha taratibu zikiwa zimewekwa chapa bandia ya dawa za kuogedha mbwa na paka kuepuka kubainika.
Kamishna Jenerali Lyimo amesema kukamatwa kwa kwa dawa hizo ni ishara ya uwepo wa tatiz la matumizi holela ya dawa za tiba zenye asili ya kulevya.
“Hii inachangiwa na kuimarika kwa udhibiti wa dawa za kulevya na kusababisha wafanyabiashara na watumiaji kutumia dawa tiba ya kulevya kama mbadala wa dawa za kulevya,” amesema.
Licha ya mbinu nyingi kutumiwa na wafanyabiashara wa dawa za kulevya kuingia nchini ikiwemo kutoa rushwa, amesema DCEA imejipanga kuhakikisha mbinu zote zinadhibitiwa.
Mikakati ya kudhibiti uingizwaji wa dawa za kulevya nchini amesema ni pamoja na Kushirikisha Taasisi ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) pamoja na kufunga Scanner maalum mipakani kwa ajili ya ukaguzi wa dawa za kulevya zinazofichwa kwenye mizigo.
“Afisa atakayehusika na ukaguzi akibainika amepitisha dawa za kulevya atawajibishwa mara moja,” amesema.
Na kuongeza katika maeneo mbalimbali nchini kupitia oparesheni za kanda, wamefanikiwa kukamata kilo 303.553 za bangi, gramu 103.8 za heroin na kilo 63 za mirungi.