Mashirika kadhaa ya ndege yamesitisha safari za kuelekea Haiti baada ya ndege ya abiria kutoka Marekani kupigwa risasi ilipokuwa ikijaribu kutua Port-au-Prince.

Ndege ya Spirit Airlines 951 kutoka Fort Lauderdale huko Florida ilielekezwa katika nchi jirani ya Jamhuri ya Dominika, ambako ilitua salama katika Uwanja wa Ndege wa Santiago.

Mhudumu wa ndege alipata majeraha madogo lakini hakuna abiria aliyejeruhiwa katika shambulio hilo, la pili katika wiki tatu kwenye ndege iliyokuwa ikiruka juu ya mji mkuu wa Haiti.

Tukio hilo linakuja wakati waziri mkuu mpya akichukua madaraka katika nchi hiyo iliyokumbwa na mzozo, ambayo imekuwa ikikumbwa na magenge yenye silaha na ghasia zinazozidi kuongezeka.

Alix Didier Fils-Aimé alisema kipaumbele chake ni “kurejesha usalama”, kulingana na shirika la habari la AFP.

Licha ya “mazingira magumu” ya nchi, aliahidi kuweka nguvu zake zote, ujuzi na “uzalendo katika kutumikia kazi ya kitaifa”.

Ndege ya Shirika la Ndege la Spirit ilikuwa inatazamiwa kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Toussaint Louverture kabla ya saa 12:00 (17:00 GMT) ilipopigwa.

Video ambayo haijathibitishwa ya tukio hilo iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii ilionekana kuonesha matundu mengi ya risasi ndani ya ndege, ambapo wafanyakazi huketi wakati wa kuruka na kutua.

Shirika la Ndege la Spirit lilisema kuwa kulikuwa na uharibifu “sambamba na milio ya risasi” wakati ndege hiyo ilipokaguliwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Santiago.

Shirika hilo la ndege lilisema pia limesitisha safari za ndege kwenda Haiti “kusubiri tathmini zaidi”.