Mwandishi wa habari aliyefungwa katika jela ya Eritrea kwa miaka 23 bila kushtakiwa ameshinda tuzo ya haki za binadamu ya Sweden kwa kujitolea kwake kwa uhuru wa kujieleza.
Dawit Isaak, ambaye ana uraia wa Eritrea na Sweden, alipewa Tuzo ya Edelstam “kwa… ujasiri wake wa kipekee”, ilielezwa katika taarifa.
Dawit, ambaye ana uraia wa nchi mbili za Eritrea na Sweden, alikuwa mmoja wa waanzilishi wa Setit, gazeti la kwanza huru la Eritrea.
Aliwekwa kizuizini mwaka wa 2001 baada ya gazeti lake kuchapisha barua zinazodai mageuzi ya kidemokrasia.
Dawit alikuwa miongoni mwa kundi la watu, wakiwemo mawaziri wakuu wa baraza la mawaziri, wabunge na waandishi wa habari huru, waliokamatwa katika msako wa serikali.
Kwa miaka mingi, serikali ya Eritrea haijatoa taarifa zozote kuhusu aliko au afya yake, na wengi waliokuwa jela pamoja naye wanadhaniwa kuwa wamekufa.
Tuzo ya Edelstam, iliyotolewa kwa ujasiri wa kipekee katika kutetea haki za binadamu, itatolewa tarehe 19 Novemba huko Stockholm.
Binti wa Dawit, Betlehem Isaak, atapokea tuzo hiyo kwa niaba yake huku akiendelea kuwa gerezani nchini Eritrea.
Kazi yake na Setit ilijumuisha ukosoaji wa serikali na wito wa mageuzi ya kidemokrasia na uhuru wa kujieleza, hatua ambazo zilisababisha kukamatwa kwake katika kukabiliana na upinzani.
Wakfu wa Edelstam umetoa wito wa kuachiliwa kwa Dawit, na kuzitaka mamlaka za Eritrea kufichua alipo na aweze kupata uwakilishi wa kisheria.
“Dawit Isaak ndiye mwandishi wa habari aliyezuiliwa kwa muda mrefu zaidi duniani. Tuna wasiwasi mkubwa kuhusu afya yake na hajulikani aliko, hakushitakiwa kwa kosa la jinai, na amenyimwa fursa ya kuonana na familia yake, usaidizi wa kibalozi na haki ya wakili wa kisheria, Caroline Edelstam, mwenyekiti wa waamuzi katika Tuzo la Edelstam alisema.