Rais wa Urusi Vladimir Putin amempongeza Donald Trump kwa ushindi wake wa uchaguzi, akimtaja kuwa “mtu jasiri”.

Akizungumza katika hafla moja katika mji wa Sochi nchini Urusi, Putin alisema kuwa Trump “alidhulumiwa kutoka pande zote” katika muhula wake wa kwanza katika Ikulu ya White House.

Putin pia alisema kuwa madai ya Trump kwamba anaweza kusaidia kumaliza vita nchini Ukraine “yanastahili kuzingatiwa”.

Wakati wa kampeni yake, Donald Trump alisema mara kwa mara kwamba anaweza kumaliza vita hivyo “kwa siku” lakini hajawahi kufafanua jinsi angefanya hivyo.

Wakati wa hotuba hiyo, Putin alizungumza kwa saa kadhaa akiangazia mada tofauti. Pia alizungumzia jaribio la kumuua Donald Trump mwezi Julai, akisema “lilimvutia sana”.

Baada ya kupigwa risasi, Trump aliinua mkono akiwa amekunja ngumi hewani na kusema maneno “pigana, pigana, pigana”, kabla ya kuondolewa katika eneo la tukio na maafisa wa huduma ya usalama wa viongozi (Secret Service).

“Kwa mtazamo wangu, alionyesha ujasiri,” Putin alisema.

Alipoulizwa ikiwa yuko tayari kufanya mazungumzo na Donald Trump, Putin alijibu: “Tuko tayari, tuko tayari.”

Siku ya Alhamisi Trump alikuwa tayari amesema kwamba yuko tayari kuzungumza na Putin, akiiambia NBC News: “Nadhani tutazungumza”.

ENDELEA KUTUFUATILIA KWENYE CHANNEL YETU YA WHATSAPP ILI KUPATA TAARIFA ZAIDI
https://spoo.me/KM4fpz