Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

MWENYEKITI wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile ameeleza kusikitishwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa kutokuhudhuria matukio mbalimbali ya kihabari ambayo anaalikwa.

Balile ameyaeleza hayo leo Novemba 07, 2024 wakati wa Mkutano Mkuu nane wa Jukwaa hilo ambapo walimualika Waziri Silaa kama mgeni rasmi lakini hakufika na kuwakilishwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Nicholas Mkapa.

“Tunasikitishwa na mwenendo wa Waziri wetu huyu ambaye mara kadhaa tumekuwa tukimualika katika matukio yetu ya kihabari kama mdau muhimu lakini hajawahi kuhudhuria.

“Hili litakuwa tukio la nne tunamualika hafiki. Alialikwa kuhudhuria Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari (EJAT) zilizotolewa Septemba 28, 2024 hakufika, hakuonekana kwenye kikao cha Jumuiya wa Maofisa Uhusiano PRST jijini Arusha na tukasikia aliitwa Mbeya hakwenda na leo kwenye mkutano huu tumemualika haijafika,” amesema Balile na kuongeza:

“Mwenendo huo haufurahishi, Waziri Silaa anapaswa kutambua tasnia ya habari ni sehemu ya wadau wake muhimu anaopaswa kushirikiana nao kwa ukaribu,”.

Hata hivyo, amemshukuru Waziri huyo kwa kuteua bodi ya ithibati inayokwenda kuleta utekelezaji wa sheria ya huduma za habari hatua aliyoichukua baada ya kuingia madarakani.

Hata hivyo ametoa wito kwa serikali kuandaa utaratibu wa wahariri kukutana na Mawaziri kama ambavyo Msajili wa Hazina huwakitanisha na mashirika na taasisi za umma.

Hata hivyo amebainisha changamoto zinazowakabili ikiwemo Sheria ya mwaka 2016 ya Huduma za Habari iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2023 akisema kuna baadhi ya mambo yanapaswa kurekebishwa.

“Pia kuna sheria ambayo inamtaka mwekezaji wa chombo cha habari kutoka nje amiliki asilimia 49 na mwekezaji wa ndani asilimia 51. Hii inawafanya wawekezaji wa nje washindwe kuja nchini kuwekeza katika sekta hii. Lakini pia mamlaka aliyopewa Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo ni makubwa,” amesema Balile.

Hata hivyo, ameipongeza Serikali kwa usimamizi bora uliopelekea Tanzania kupanda katika uhuru wa vyombo vya habari duniani hadi kufikia nafasi ya 97 kutoka 143 katika uhuru wa vyombo vya habari duniani.

Akifungua mkutano huo kwa niaba ya Waziri Silaa, Mkapa amesema serikali itaendelea kushirikiana na vyombo vya habari nchini pamoja na kufanyia mapitio ya sera mbalimbali zinazohusu vyombo vya habari.

Amesema vyombo vya habari vina umuhimu mkubwa nchini kwani ni daraja kati ya serikali na jamii.

“Tunawapongeza wahariri kwa kazi kubwa ambayo mnaifanya. Tunawaomba muendelee kuzingatia weledi, maadili pamoja na kudumisha amani iliyopo.

“Sisi kama serikali tunaendelea kushughulikia changamoto mbalimbali zilizopo pamoja na kufanyia marekebisho sera mbalimbali ambazo zimekuwa kukwazo katika utendaji wenu wa kazi,” amesema Mkapa.

Mkuu wa Ilala, Edward Mpogolo amesema wataendelea kushirikiana na vyombo vya habari katika kutatua changamoto zinazojitokeza wakati wa utekelezaji wa majukumu kwa maslahi mapana ya Taifa.

“Tunawashukuru kwa kazi kubwa mnayoifanya, ombi langu tuendelee kushirikiana na sisi serikali na tuko tayari kupokea maoni na kuyafanyia kazi.

“Vyombo vya habari vina nafasi kubwa kwenye maadili yetu. Hivyo tuendelee kuzingatia amani kwani ni jambo la muhimu sana, mchakato wa amani unajengwa na huwezi kuzungumzia amani bila haki na upendo,” amesema Mpogolo.