na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia

Wataalam Tume Ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), wamekumbushwa kuzingatia sheria na kanuni mpya za manunuzi katika usimamizi wa miradi na utekelezaji wa manunuzi.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Raymond Mndolwa, wakati wa mafunzo ya siku tano ya Sheria Mpya ya Manunuzi ya Umma Namba 10 ya Mwaka 2023 na Kanuni za mwaka 2024,iliyowahusisha Afisa Masuuli, Wajumbe wa Bodi ya Zabuni na Wahandisi wa Mikoa.

“Wakati mwingine sisi watumushi wa serikali tunakuwa sababu ya wakandarasi kuisababishia hasara serikali”, ameongeza Mndolwa

Mndolwa amesema, lengo la kutoa elimu hiyo juu ya sheria mpya ni kuhakikisha wataalamu hao wanazingatia sheria na taratibu sahihi ili kuepusha hasara za manunuzi kwa serikali.

“Ndani ya kazi ya umma hakuna nia njema kuna utaratibu, niwaombe sana tufuate taratibu tusimamie kazi zetu, hii sheria ambayo mnakumbushwa mjione ninyi ni watendaji wakuu katika mikoa yenu,” alisema Mndolwa.

Amesisitiza kuwa ni muhimu kwa wataalamu wanaosimamia miradi ya serikali, kuhakikisha hawafanyi kazi ya kushirikiana na wakandarasi kuihujumu serikali.

Aidha, amesema kuwa miradi mizuri ya umwagiliaji lazima idumu kwa muda mrefu na ili kudumu inahitajika umakini kuzingatia sheria na kanuni.

“Mradi mzuri wa umwagiliaji lazima uishi sio chini ya miaka 20 bila ukarabati, mjiulize maswali mnaosimamia miradi je mradi ninaosimamia utadumu zaidi ya miaka 20 bila ukarabati.”

Pia Mndolwa, alihimiza wahandisi na wataalamu wa manunuzi kuhakikisha kuwa mikataba ya manunuzi inasimamiwa kwa umakini.

“Rais wetu Dkt Samia Suluhu Hassan, kwa sasa katika hotuba zake kila baada ya maneno kadhaa anapozungumzia uchumi na kufikia kuilisha dunia lazima anasisitiza kuhusu umwagiliaji”, ameongeza Mndolwa

“Umwagiliaji ni NIRC hivyo wahandisi wetu wa mikoa mna wajibu wa kuepusha serikali na hasara zisizohitajika na kuisaidia serikali kufikia malengo ya kiuchumi,”amesisitiza.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi NIRC Yahaya Amour Omary amesema mafunzo hayo, yanaendeshwa na wataalamu kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) na yamelenga kuongeza uelewa kwa wataalamu hao wa Tume kuhusu sheria mpya ya manunuzi na kuhakikisha malengo ya Tume katika miradi ya kimkakati yanafikiwa.

Yahya ameongeza kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za Mkurugenzi Mkuu NIRC kushirikisha PPRA katika kuwajengea uwezo watumishi wa Tume wanao husika katika mchakato wa Manunuzi na usimamizi wa miradi inayoendelea.

Baadhi ya Wahandisi wa umwagiliaji na wataalam wengine wanaoshiriki mafunzo hayo akiwemo Banzi Abdallah Nassoro wameeleza matarajio yao baada ya mafunzo ikiwemo kuongeza uwezo na bora wa kusimamia miradi yenye tija na kufikia azma ya serikali.

Naye Mhandisi wa Mkoa wa Ruvuma Lusia Chaula amesisitiza kuwa mafunzo hayo ni muhimu katika kuwezesha utendaji kazi wao hasa katika mchakato wa masuala ya manunuzi, kuongeza ufanisi, tija na kuiepusha serikali hasara.