Na Lookman Miraji, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Tasnia ya filamu nchini kupitia kampuni ya uandaji filamu ya Allan Cultural group (ACG) imedhamiria kutoa elimu ya saratani kupitia fani sanaa.
Hatua hiyo imekuja mara baada ya kampuni hiyo kutangaza rasmi ujio wa filamu mpya ya “PIGO” ambayo inatarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni ambapo filamu hiyo itahusisha utoaji wa elimu juu ya ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi.
Akizungumza leo hii katika mkutano na wanahabari Mkurugenzi wa kampuni ya uandaaji filamu ya Allan, Bi: Mwaija Mungi amesema kuwa hatua ya kuandaa mradi wa filamu hiyo imekuja ili kuunga mkono jitihada kubwa zinazofanywa na serikali katika kupambana na ugonjwa wa saratani nchini kupitia utoaji elimu kwa jamii.
“Sisi kama Allan tumeguswa na jambo hili na sisi tumeona tuwe sehemu ya wale watu ambao wanaweza kutoa elimu hii kwa jamii”
Aidha Bi: Mwaija Mungi ameongeza pia mradi wa filamu hiyo utaenda sambamba na utoaji wa huduma za tiba kwa magonjwa mbalimbali yasiyoambukiza ili kuhamasisha jamii juu ya upimaji afya mara kwa mara.
“Pia tutaenda sambamba na kutoa huduma ya tiba shufaa kwa magonjwa yasiyoambukiza lakini pia tutaendesha zoezi la upimaji wa saratani ya tezi dume na saratani ya matiti. Kwahiyo katika kuliendea jambo hilo tutakuwa tumeungana moja kwa moja na madaktari wetu ili kuweza kuleta huduma hiyo karibu kwa jamii iliyolengwa” Alisema.
Kwa upande mwingine pia bodi ya filamu kupitia Afisa mwandamizi wa maendeleo ya filamu nchini, Clarence Venance nae amepongeza hatua hiyo iliyofanywa na kampuni ya Allan kwani itasaidia watu wengi kuelimika na kutambua njia sahihi ya kukabiliana na changamoto ya ugonjwa huo.
Pia Afisa huyo ametoa wito kwa kampuni nyingine za uandaaji filamu kubuni mawazo mengine yakayotumia sanaa kuelimisha jamii ya kitanzania.
Mradi wa filamu hiyo ya “PIGO” utahusisha jumla ya mikoa 13 nchini huku ukihamasishwa na michezo kupitia kombe la Allan litakalohusisha timu za mchangani kutoka sehemu mbalimbali.
Filamu hiyo inatarajiwa kuzinduliwa rasmi disemba 5 mwaka huu na waziri afya nchini Dkt: Jenista Mhagama.