Na Fauzia Mussa, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 1992, inaeleza kuwa uongozi wa kisiasa ni moja ya mlango mkubwa na njia muhimu ya kuwa kiongozi mwenye fursa ya kutoa maamuzi katika nchi.
Hadi sasa kuna vyama vitatu tu sawa na asilimia 16 vilivyosimamisha miili ya wanawake kushika wadhifa wa ukatibu Mkuu wa vyama vyao kati ya vyama 19 vilivyosajiliwa, na wanawake wanne ndio manaibu katibu kati ya manaibu wasaidizi 38 wa vyama hivyo sawa na asilimia 14, hali inayoonesha kupewa mgongo matakwa ya Katiba ya jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 Ibara 21 (1) (2) inatoa fursa kwa raia wote kushiriki katika maswala yanayohusu uongozi, na inayoeeleza zaidi kuwa binadamu wote wamezaliwa huru na wote ni sawa.
Vyama vya siasa vina nafasi kubwa ya kumwezesha mwanamke kuwa kiongozi ndani na nje ya chama endapo vitakua vinafuata vyema miongozo inayotoa kipaombele kwa wanawake kushika nafasi hizo.
Makala hii itazungumzia namna vyama vinavyosaidia wanawake kushika nafasi za uongozi ikiwemo matakwa ya katiba za vyama zao.
VYAMA VYENYEWE VINAELEZA
CHAMA CHA MAPINDUZI
Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Zanzibar, Khamis Mbeto Khamis, anasema kuwa chama hicho kinaongozwa na katiba na maelekezo ambayo moja kwa moja yanampa fursa mwanamke anaejiamini kuwa kiongozi.
“Katiba ya chama chetu ya mwaka 1977 Toleo la Disemba 2022 inaeleza kuwa binaadamu wote ni sawa na pia miongozo inaelekeza kuwa kila kada wa chama hichi ana haki sawa katika kuchaguwa na kuchaguliwa.” Alisema Mbeto
Mbeto anasema pamoja na hayo chama kinachukua juhudi za kuwajengea uwezo wanawake kupitia mafunzo na kuwaandaa kwenye mabaraza ya vijana ili kuwa na viongozi bora wa jinsia hiyo watakaoiamanishia dunia kuwa nao wanaweza, “ hatua zote hizi zinachangia uwepo wa miili ya wanawake waliyo na utayari kushika nafasi za uongozi ndani ya Chama na Serikali.” alisema Mbeto.
ACT WAZALENDO
Fatma Alhabib Fereji ni Katibu Ngome ya Wanawake Taifa wa chama cha Act Wazalendo anasema kuchagua na kuchaguliwa ni haki ya kila mwanachama bila kujali jinsia kwa mujibu wa imani ya chama chao.
“Katiba yetu toleo la 2024, suala la usawa kijinsia katika nafasi za uongozi ni jambo la lazima, mfano uk. 7-8 wa katiba yetu unaeleza kati ya wajumbe 10 wa mkutano Mkuu, theluthi moja iwe ni wanawake kadiri inavyowezekana, uk 21 kf 39 (h) toleo hilohilo unasema kutakuwa na wajumbe wanne wakuchaguliwa wakiwemo wanaume wawili na wanawake wawili na kf 63 (h) (i) kinaeleza wajumbe 2 wa mkutano mkuu (diaspora), mmoja awe mwanamke, hali hii inaonesha matakwa ya katiba yanavyolazimisha uwiano katika uongozi”. Alifafanua Fatma Fereji
Mwanangome huyo Alibainisha nafasi za uongozi zilizoshikwa zilizoshikwa na wanawake katika chama hicho kuwa ni pamoja na wanawake 9 kati ya wajumbe 17 wa Sekratirieti ya Taifa, sawa na asilimia 53, wanawake watatu kati ya wajumbe 12 wa kamati ya uongozi Taifa sawa na asilimia 25, wanawake 23 kwenye kamati kuu kati ya wajumbe 55 sawa na asilimia 42, wanawake 27 kati ya wajumbe 126 wa halmashauri kuu sawa na asilimia 21, wanawake 6 kati ya wajumbe 9 wa bodi ya wadhamini sawa na silimia 66, wanawake 23 kati ya mawaziri 25 wa baraza kivuli la mawaziri sawa na asilimia 52, na wanawake 21 kati ya manaibu waziri kivuli 47 sawa na asilimia 45, Takwimu zianzoonesha bado nguvu zinahitajika kufikia 50 kwa 50 katika kila panahitaji kiongozi.
CHAMA CHA MAKINI
Katibu wa Chama cha Makini, Ameir Hassan Ameir, naye anaeleza kuwa chama hicho kina jumla ya viongozi wakuu 10, sita kati ya viongozi hao ni jinsia ya kike, anasema kuwa hali hiyo inatokana na katiba na kanuni za chama hicho kuwa na nguvu ya kuhakikisha wanawake wanashika hatamu ya uongozi ndani na nje ya Chama.
“Nathubutu kusema kuwa Asilimia 70 ya viongozi katika chama hichi ni wanawake na asilimia zilizilozibakia ndio jinsia ya kiume.” Alikazia kiongozi huyo
CHAMA CHA WANACHI CUF
Amina Rashid Salim (47), mwananchama wa chama hicho Jimbo la shauri moyo Wilaya ya Mjini, Mjumbe wa mkutano mkuu Wilaya, mjumbe mkutano mkuu Taifa Chama, Mkutano Mkuu Taifa Jumuiya ya Wanawake na ofisa Mipango na Chaguzi Taifa anasema ameshika nafasi zote hizo ni kutokana na chama hicho kuamini jinsia zote zina haki sawa.
Mbali na hayo Amina anasema wanaongozwa na katiba na kanuni zinazomweka huru mwanamke kuwa kiongozi, kutengeneza usawa wa kijinsia na kuuwa dhana za ubaguzi.
“Kf nm 2 (d) cha katiba ya Chama chetu kinaeleza kuwa kati ya wajumbe 10 wa kamati tendaji ngazi ya tawi lazima watatu wawe ni wanawake, kifungu na (57) (3) kimeelekeza kati ya wajumbe wasipoungua 7 na wasiozidi 9 wa kamati tendaji ngazi ya jimbo, watatu lazima wawe wanawake, kf 62 (2e), kinaeleza kuwa kati ya wajumbe 15 ngazi ya wilaya angalau au wasiopungua 5 wawe ni wanawake, na kf 78 (m) (n) (o) kinaelekeza kuwa kati ya wajumbe 20 ngazi ya Taifa wajumbe wasiopungua 6 wawe wanawake.” aligusia Amina
MTAZAMO WA WANAHARAKATI NA WADAU
Mchambuzi wa mambo ya kisiasa, Almas Mohammed, anasema licha ya katiba na sheria za nchi kutoa fursa sawa kwa jinsia zote kugombea nafasi za urais, ubunge, uwakilishi na udiwani lakini miongozo iliyopo kwa kiasi kikubwa imeupa mgongo usawa wa kijinsia, hauzingatii hali halisi ya ushiriki wa wanawake kwenye michakato ya maamuzi. “Wanawake wachache waliobahatika kuingia kwenye duru za uongozi kupitia uteuzi basi si kwa sababu ya maelekezo ya kisheria” alikazia mchambuzi huyo
Anasema kuja marekebisho ya sheria ya vyama vya siasa ya 2024 yaliyoongeza kifungu cha 10 (c) kinachovitaka vyama kuwa na nyaraka zinazojumuisha sera ya jinsia na mjumuisho wa kijamii yameleta faraja kidogo na kutia moyo wa kuweza kufikia 50 – 50 katika nafasi za uongozi.
Hata kwenye utumishi wa umma, wanawake wanatakiwa kujituma na kufanya kazi kwa uweledi ili kupanda vyeo au madaraja. “Uteuzi na upandishaji wa vyeo katika utumishi wa umma utafanywa kwa kuzingatia sifa na uwezo” Sheria ya Utumishi wa Umma (2011) katika kifungu cha 5 (2b) inaeleza.
Mkurugenzi TAMWA –ZNZ, Dk. Mzuri Issa anasema kutokana na kuwa Tanzania imeridhia mikataba na matamko mbalimbali ya Kimataifa inayotoa haki kwa kila mtu kushiriki katika utawala wa nchi, ni wakati wa kufikia 50 kwa 50 katika ngazi za maamuzi.
“ Tamko la Kimataifa kuhusu Haki za Binadamu (UDHR: 1948), Mkataba wa Kimataifa wa kutokomeza aina zote za ubaguzi dhidi ya wanawake (CEDAW: 1979, Ibara namba 7: a,b na c), Mapendekezo ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC 1325(2000) Mpango Kazi wa Beijing (1995), Malengo ya Millenia ya Maendeleo (Lengo la 13), pamoja na Mkataba wa Afrika kuhusu haki za Binadamu ikiwa ni pamoja na Mkataba wa Ziada wa Maputo, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) pamoja na mapendekezo ya Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (2014/15)pamoja na Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia (URT: 2000) zote hizo zimebainisha haki za wanawake kushiriki katika nafasi mbalimbali za uongozi.” Alinukuu Dk. Mzuri.
SHERIA ZINASEMAJE
Ofisa sheria Mwandamizi kutoka ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa, Abdulrazak Ali anasisitiza kuwa suala la usawa wa kijinsia ni jambo lisilopingika na kuwa kuna umuhimu wa vyama vya siasa kuzingatia na kusimamia hilo kwa kuandaa miongozo imara itakayosimamia maadili na kukemea vitendo vya unyanyasaji hali itakayowasaidia wanawake kuwania nafasi mbalimbali za uongozi na kuongoza.
Anasema Katiba ya Zanzibar, ibara ya 21(1), sheria ya vyama vingi ya mwaka 1992 na sheria ya chaguzi za serikali za mitaa ya mwaka 1982 zinatilia mkazo juu ya haki za raia kushiriki katika harakati za kisiasa.
“Katiba ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ibara ya 5(1) mtu yeyote bila kujali jinsia (mwanaume au mwanamke) mwenye umri usiopungua miaka 18 ana haki ya kuchagua au kuchaguliwa kuwa kiongozi (Ibara ya 5(1)).” Aliongeza mtaalamu huyo
MWELEKEO THABITI WA USAWA WA KIJNSIA
Lau kama sheria zote zinazotoa fursa ya uongozi zingefuata mwelekeo wa sheria ya Baraza la Vijana la Taifa (2014), bila ya shaka sura ya uwakilishi wa wanawake katika uongozi na siasa ingekuwa tofauti sana na ilivyo leo.
kifungu cha 10 (1a) cha sharia hiyo kinaainisha wajumbe wa Baraza la Taifa ambao ni Mwenyekiti, Katibu, Wajumbe 3 kutoka kila baraza la wilaya, Wajumbe 3 kutoka kila baraza la Mkoa, na kutoa amri ya kisheria juu ya kuzingatia jinsia.
Aidha, vifungu vya 10 (4d), 12 (2d) na 17 (2d) vinataja juu ya vyombo vya utendaji wa baraza kutoka ngazi ya shehia hadi taifa na kueelekezwa kuwa katika wajumbe 7 wa vyombo hivyo, angalau 3 wawe wanawake