Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Thabit Kombo tarehe 05 Novemba, 2024 ametembelea Maonesho ya Kimataifa ya Biashara yanayoendelea jijini Havana.
Maonesho hayo yamewakutanisha wafanyabiashara wa ndani na Kimataifa ambao wanatangaza huduma na bidhaa zao ili kuongeza wateja, kukuza soko, kuboresha huduma pamoja na kupeana uzoefu na wafanya biashara wengine.
Miongoni mwa mabanda aliyoyatembelea Waziri Kombo ni pamoja na banda la Kampuni ya LABIOFARM iliyowekeza nchini kwa kujenga kiwanda cha viuadudu kwa ajili ya kudhibiti malaria kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) kilichopo Kibaha, Pwani.
Kampuni hiyo pia kupitia miundombinu iliyopo ina uwezo wa kuzalisha mbolea na viwatilifu hivyo, itasaidia kuondoa changamoto katika shughuli za kilimo na kuongeza ajira kwa watanzania na wacuba.
Mabanda mengine ni pamoja na kampuni ya Kimataifa ya Havana Club ambayo inazalisha na kuuza vinywaji mbalimbali ikiwemo mvinyo na vinywaji vikali. Tayari kampuni hiyo imeonesha nia ya kuongeza mauzo yake nchini Tanzania na kupata wasambazaji zaidi.