• Ajira zamwagwa kwa Watanzania, Minada ya Madini kurejeshwa, Mauzo yapaa

Na Vicky Kimaro- Tume ya Madini

“Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika Sekta ya Madini, tumenunua mitambo mikubwa, mitano imeshafika nchini, kumi ipo njiani inakuja, mitambo hii itawarahisishia wachimbaji wadogo kupata taarifa za uchimbaji na kuwaepusha na hasara,” kauli ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliyoitoa Oktoba 21, 2024 ambapo aliongeza,

“Mitambo hii ikifika itagawanywa pote, ila nimemtaka Waziri (Mheshimiwa Anthony Mavunde) atenge mitambo miwili kwa ajili ya vijana na mmoja kwa ajili ya wanawake.

Kauli hiyo ya Rais Samia ni muendelezo wa dhamira yake ya dhati ya kuhakikisha Sekta ya Madini inaendelea kuongeza mchango wake katika ukuaji wa uchumi wa nchi.

Mpango wa Serikali ni kuhakikisha kuwa sekta hii inachangia asilimia 10 au zaidi katika Pato la Taifa ifikapo 2025.

Ukuaji wa Sekta ya Madini umeongezeka kutoka asilimia 9.4 Mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 11.3 Mwaka 2023 kutokana na kuendelea kuimarika kwa Sekta, Mchango wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa utaongezeka na kufikia asilimia 10 au zaidi ifikapo Mwaka 2025 kama ilivyoelezwa katika Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025.

Uboreshaji wa sheria, kanuni na miundombinu ikiwemo ya umeme migodini, ndani ya miaka mitatu ya Rais Samia Suluhu Hassan, kupitia Tume ya Madini kiwango cha makusanyo ya maduhuli ya Serikali kimepanda kutoka Shilingi bilioni 624.61 zilizokusanywa Mwaka wa Fedha 2021/2022 hadi kufikia Shilingi bilioni 753.82 Mwaka wa Fedha 2023/2024, makusanyo hayo ni sawa na ongezeko la asilimia 20.7 ya makusanyo kwa miaka mitatu.

“Mathalani katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025 ambapo tulipewa lengo la kukusanya shilingi Trilioni Moja, hadi kufikia Oktoba 21, 2024 Tume ya Madini imefanikiwa kukusanya Jumla ya Shilingi bilioni 312.75 sawa na asilimia 31.28 ya lengo la mwaka,”anasema Mhandisi Ramadhani Lwamo, Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini hivi karibuni katika kikao chake na Wahariri wa Vyombo vya Habari.

Mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 7.2 Mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 9.0 Mwaka 2023 hiyo ni kutokana na kuimarika kwa usimamizi wa shughuli mbalimbali za madini nchini.

MAUZO YA MADINI YAPAA

Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini kwa kushirikiana na Mamlaka za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa nchini imeendelea kusimamia utendaji kazi wa Masoko ya Madini na vituo vya ununuzi wa Madini nchini.

“Katika Mwaka wa Fedha 2023/2024 mauzo ya madini katika Masoko na Vituo vya Ununuzi wa Madini yalikuwa Shilingi bilioni 2,592.02 na mapato yaliyopatikana kutokana na mauzo hayo ni kiasi cha Shilingi bilioni 180.13 ikilinganishwa na Mwaka wa Fedha 2021/2022 ambapo ilikuwa Shilingi bilioni 2,361.80,”amesema Mhandisi Lwamo na kuongeza

“Mapato ya Serikali yaliyopatikana ni Shilingi bilioni 164.09 ambapo mapato hayo yalihusisha mrabaha na ada ya ukaguzi wa madini nchini,”amesema Mhandisi Lwamo.

UELEKEO SEKTA YA MADINI

Uelekeo wa Sekta ya Madini katika kuchangia Pato la Taifa ili kufikia asilimia 10 au zaidi ifikapo mwaka 2025 kama inavyofafanuliwa katika Dira ya Maendeleo ya Taifa, Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 pamoja na Mpango Mkakati wa Tume ya Madini wa Mwaka 2024/2025, 2025/2026, Tume ya Madini imeweka mikakati endelevu ikiwemo kuimarisha usimamizi na udhibiti katika maeneo ya uzalishaji wa madini ujenzi na madini ya viwandani kwa kuongeza Wakaguzi Wasaidizi wa Madini Ujenzi (AMAs), vitendea kazi (PoS) pamoja na kushirikisha Mamlaka nyingine za Serikali zinazosimamia na kutumia rasilimali hizi (Halmashauri, Polisi, TARURA na TANROADS) lengo ni kuongezeka kwa makusanyo yatokanayo na rasilimali ya madini ujenzi na madini ya viwandani.

Pia, mkakati mwingine ni kuimarisha udhibiti wa biashara haramu ya madini hususan utoroshaji wa madini kwa kuhamasisha umuhimu wa kutumia Masoko na vituo vya madini nchini; kuimarisha vituo vya ukaguzi (exit-points) katika maeneo ya mipakani, bandarini pamoja na viwanja vya ndege lengo likiwa ni kupunguza matukio ya utoroshaji wa madini na hivyo kuwezesha Serikali kupata takwimu sahihi na mapato stahiki.

Pia, uboreshaji na usimamizi thabiti wa mfumo wa utoaji wa leseni za madini, matokeo ni kupunguza migogoro itokanayo na mwingiliano wa maombi ya leseni, kupunguza muda wa utoaji huduma pamoja na kuongeza idadi ya leseni zitakazotolewa kwa mwaka hivyo kuhamasisha uwekezaji.

Mkakati mwingine ni kuimarisha ukaguzi katika shughuli za uchimbaji katika migodi kwa lengo la kuwa na uchimbaji endelevu unaozingatia usalama, afya na mazingira, lengo kuongeza mapato, kuimarisha uchimbaji endelevu unaojali mazingira kwa manufaa ya vizazi vilivyopo na vijavyo.

Pia, kuimarisha Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa (RMOs) na Maabara katika maeneo mbalimbali ya uzalishaji hapa nchini, lengo likiwa ni kusogeza huduma karibu na wadau hivyo kuchochea uwekezaji utakaowezesha Serikali kuongeza mapato yatokanayo na rasilimali madini.

Mikakati mingine ni pamoja na kuimarisha shughuli za tafiti zinazohusiana na utambuzi wa vyanzo vipya vya mapato yatokanayo na rasilimali za madini, lengo likiwa ni kuiwezesha Taasisi kuongeza wigo wa makusanyo yatokanayo na rasilimali madini ikiwemo kuimarisha mazingira ya uwekezaji kwa wachimbaji wa madini ili kuongeza mapato, ajira na kuwa sekta endelevu.

WATANZANIA KUNUFAIKA NA MADINI

Tume ya Madini katika kuhakikisha kuwa Wananchi wananufaika na rasilimali madini, imeendelea kusimamia uwasilishaji wa Mipango ya Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini (LCPs) kutoka kwa Wamiliki na Waombaji wa leseni za madini pamoja na watoa huduma kama takwa mojawapo la Sheria ya Madini Sura ya 123.

Katika kipindi cha Mwaka 2021 hadi kufikia Mwaka 2023, jumla ya Mipango 1,050 ya Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini ilipokelewa na kufanyiwa uchambuzi. Kati ya Mipango iliyowasilishwa, 1,036 ilikidhi vigezo na kuidhinishwa na Mipango 14 haikukidhi vigezo hivyo ilirejeshwa kwa wahusika kwa ajili ya marekebisho.

AJIRA ZA WATANZANIA ZAONGEZEKA

Tume ya Madini imeendelea kusimamia kikamilifu upatikanaji wa ajira kwa Watanzania kutoka kwenye Makampuni mbalimbali ya Uchimbaji ambapo katika kipindi cha mwaka 2021 hadi 2023 Kampuni ziliweza kuzalisha ajira 19,356 ambapo kati ya hizo 18,853 ni Watanzania sawa na asilimia 97.40 na 503 ni wageni sawa na asilimia 2.60 ya ajira zote zilizozalishwa.

Vilevile, jumla ya bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani (USD) 3,780,161,183.28 ziliuzwa na kusambazwa migodini ambapo kati ya bidhaa hizo Kampuni za Watanzania zilifanikiwa kuuza bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani (USD) 3,465,592,451.28 sawa na asilimia 91.68 ya thamani ya mauzo ya bidhaa zote na huduma zilizotolewa migodini.

LESENI LUKUKI ZATOLEWA:

Tume ya Madini imekuwa ikitoa leseni za uendeshaji wa shughuli za madini kwa wadau wake kwa kuzingatia Sheria ya Madini Sura 123. Katika kuendelea kuimarisha uwekezaji katika Sekta ya Madini nchini, katika kipindi cha kuanzia 2021/2022 hadi 2024/2025, Tume ilikusudia kutoa leseni 37,318 hata hivyo hadi kufikia Septemba 30, 2024/2025 Tume ilifanikiwa kutoa jumla ya leseni 34,348 sawa na asilimia 92.04 kati ya leseni zilizopangwa kutolewa.

Leseni hizo zilijumuisha leseni za Uchimbaji Mkubwa, Uchimbaji wa Kati, Uchimbaji Mdogo, biashara ya madini pamoja na uchenjuaji wa madini.

Vilevile, Tume imeendelea kuimarisha mazingira ya uwekezaji mkubwa kwenye Sekta ya Madini nchini kwa kutoa leseni kubwa kwa makampuni mbalimbali ya uchimbaji wa madini.

Leseni hizo za uchimbaji mkubwa wa Madini zilitolewa kwa Faru Graphite Corporation Limited itakayojihusisha na uchimbaji wa madini ya kinywe Wilayani Mahenge yenye leseni SML- 676/2022; Mamba Minerals Corporation Limited inayojihusisha na uchimbaji wa Rare Earth Elements-REE katika eneo la Ngualla yenye leseni SML 693/2022 iliyopo mkoani Songwe.

Pia, leseni ya usafishaji madini kwa kampuni ya Tembo Nickel Refining Company Limited iliyopo katika Wilaya ya Ngara Mkoani Kagera yenye leseni SM- 651/2021; na Sotta Mining Corporation Limited iliyopo Mkoani Mwanza, Wilaya ya Sengerema yenye leseni SML-653/2021`.

KUDHIBITI UTOROSHAJI MADINI

Kuanzishwa kwa Masoko ya Madini nchini Tanzania kumesaidia kudhibiti utoroshaji wa madini na kuongeza uwazi katika Sekta ya Madini ambapo hadi sasa kuna jumla ya Masoko 44 na Vituo 106 vidogo vya ununuzi wa madini vimeanzishwa hapa nchini.

Masoko hayo yamesaidia kuweka mifumo ya kufuatilia na kusimamia biashara ya madini, ikiwemo teknolojia za kidijitali ambazo zinasaidia kurekodi taarifa za madini kutoka kwa wachimbaji hadi kwa wanunuzi.

Pia, kuanzishwa kwa Masoko hayo kumesaidia kudhibiti bei kwa kutoa bei elekezi ambazo ni shindani na za haki, sawa na soko la dunia hivyo kupunguza hamasa ya watu kutorosha madini kwa nia ya kuuza kwa bei ya juu zaidi kwenye soko la magendo.

Aidha, masoko hayo yamesaidia kuongeza mapato ya Serikali kupitia tozo na ada mbalimbali zinazotozwa kwenye masoko hayo.

MINADA YA MADINI KURUDISHWA

Serikali kupitia Tume ya Madini inarudisha minada ya ndani ya madini ya vito itakayofanyika katika maeneo ya uzalishaji hususan Mirerani, Mahenge, Tunduru, Dar es Salaam, Arusha na Tanga na kimataifa itafanyika mji wa Bangkok na Jaipur nchini India.

Uendeshaji wa minada hiyo ni fursa muhimu ya kutangaza madini ya vito yanayozalishwa hususan kwenye masoko ya kimataifa ambayo ni njia mojawapo ya kuwafikisha watanzania katika masoko ya uhakika na upatikanaji wa bei nzuri na stahiki.