Na Lookman Miraji, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Safari ya mahusiano kati ya mataifa mawili ya Tanzania na China imezidi kuvuka mipaka ya kidiplomasia hadi kufikia katika ngazi za juu zaidi ya uhusiano.
Nchi hizo mbili ziko katika maadhimisho ya kusheherekea kilele cha miaka 60 ya mahusiano ya kidiplomasia tangu mahusiano hayo yalipoasisiwa kwa mara ya kwanza mnamo mwaka 1964.
Katika kipindi chote cha miaka 60 ya uhusiano baina ya mataifa hayo mawili yameshuhudiwa mambo mengi ya msingi yaliyonufaisha nyanja mbalimbali za mataifa hayo huku Tanzania ikinufaika zaidi na uhusiano huo thabiti.
Mahusiano mazuri yaliyokuwepo yamechochea kwa kiasi kikubwa ukuaji wa sekta mbalimbali kwa taifa kwa taifa la Tanzania huku miongoni mwake ikiwa ni sekta uchumi, miundombinu, utamaduni pamoja sekta ya utalii.
Ni ukweli wa dhahiri kabisa nadiriki kusema si kazi ndogo iliyofanyika kwa serikali ya Tanzania kuhakikisha inawekeza nguvu kubwa kulinda mahusiano mazuri na taifa kubwa lililoendelea zaidi katika ramani ya kidunia.
Makala hii itaangazia mambo muhimu yatakayothibitisha usemi wa “Miaka 60 ya Tanzania na China ni zaidi Diplomasia”.
UKUAJI WA SEKTA YA UTALII.
Serikali ya Tanzania kupitia wizara yake ya maliasili na utalii inazidisha jitihada zake za kutangaza rasilimali za nchi kwaajili ya utalii.
Sekta ya utalii inatajwa kama sekta inayoongoza kiuchumi nchini ambapo kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na waziri wa utalii Balozi Pindi Chana zinasema kuwa kuanzia mwaka 2014 mpaka 2024 idadi ya watalii wa kimataifa iliongezeka kwa asilimia 59 kutoka idadi ya watu 1,140,156 hadi watu 1,808,205 huku mapato yatokanayo na utalii wa kimataifa yakiongezeka kwa asilimia 68.2 kutoka dola za kimarekani billioni 2.006 hadi kufikia dola za kimarekani billioni 3.374. Katika kipindi hiko utalii umechangia zaidi ya asilimia 25 ya mauzo ya nnje ya Tanzania na kuchangia asilimia 60 ya mapato yatokanayo na huduma nchini ambazo hutumiwa na wageni kutoka masoko mbalimbali ya utalii.
Kwa upande mataifa mawili ya China na Tanzania, takwimu zinaeleza kuwa idadi ya watalii kutoka nchini China wanaokuja kuitembelea Tanzania imeongezeka kutoka idadi ya watu 32,773 mwaka 2018 na kufikia watalii 44,438 kwa mwaka 2023. Vilevile kwa mwaka 2024 kuanzia mwezi januari hadi mwezi septemba mwaka huu, Tanzania imepokea idadi ya watalii 54,446 kutoka nchini China ikiwa ni ongezeko la asilimia 69 ukilinganishwa na kipindi hicho kwa mwaka 2023 ambapo ilipokea watalii 32,281 kutoka nchini China.
Takwimu hizo zinaelezea kwa namna kubwa jinsi mahusiano kati ya mataifa hayo mawili yalivyochochea ukuaji wa sekta ya utalii kwa taifa la Tanzania.
SEKTA YA MIUNDOMBINU.
Kwa asilimia kubwa sekta ya miundombinu ya Tanzania imekuwa mnufaika mkubwa wa mahusiano kati ya mataifa hayo mawili.
Rejea katika miaka ya 1970 , China ilifadhili ujenzi wa mradi usafirishaji wa reli ya TAZARA inayounganisha Tanzania na mataifa mengine jirani kama Zambia ambapo reli hiyo mara baada ya kukamilika kwake imesaidia vilivyo nyanja ya usafirishaji na biashara.
Bado sijamaliza, China imesaidia vilivyo ujenzi wa miundombinu katika ya michezo nchini Tanzania. Miongoni mwa miradi hiyo ni ujenzi wa uwanja wa michezo wa Amaan ulioko visiwani Zanzibar pamoja na ujenzi wa uwanja wa taifa wa kisasa (Benjamin Mkapa kwa sasa) katika kiwango cha hadhi ya olimpiki katika jiji la Dar es salaam ambao ni sehemu ya mradi mkubwa wa michezo nchini uliofadhiliwa kwa pamoja na serikali zote mbili.
SEKTA YA SANAA NA UTAMADUNI.
Katika kipindi cha miaka 60 iliyopita sekta ya sanaa na utamaduni imekuwa ikinufaika kupitia ubadilishanaji wa kazi za utamaduni, sanaa, fasihi na elimu ambapo taasisi za Confucius zimeanzishwa katika chuo kikuu cha Dar es salaam pamoja na kile cha Dodoma ili kusaidia katika kujifunza lugha za utamaduni wa kichina.
Vilevile nathibitisha hili kwa kuwa shuhuda wa kuona vikundi mbalimbali vya utamaduni vikipata nafasi ya kushiriki katika hafla za kitamaduni na sherehe zinazofanyika katika nchi hizi mbili za China na Tanzania.
Pia nimeshuhudia wataalamu wa masuala ya utamaduni na sanaa kutoka nchi hizi wakipata nafasi ya kushiriki katika programu mbalimbali nchini China ili kupata uzoefu.
SEKTA YA AJIRA.
Uwekezaji katika sekta ya ajira Tanzania imenufaika kwa kiasi chake pia ambapo kampuni kutoka nchini China zimewekeza zaidi ya dola za kimarekani billioni 11 na kutoa ajira zaidi ya 150,000 kwa watanzania ambapo jambo hilo limechangia kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi kupitia ajira.
Mbali na hayo yote niliyotangulia kuyataja hapo kubwa zaidi katika maadhimisho haya ya miaka 60 ya ushirikiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na China ni wakati ambapo Waziri wa maliasili na utalii Balozi Pindi Chana akiwasilisha salamu zake katika maadhimisho ya sherehe hizi amesema kuwa serikali ina kila sababu ya kujivunia kuona kwamba uhusiano huu wa kirafiki umekuwa ukidumu na kuimarika siku hadi siku.
“Tunapoadhimisha siku hii hatuna budi kuenzi na kuthamini juu ya safari ya kipekee tuliyofanya kwa pamoja ambapo nchi zetu zimekuwa na uhusiano ambao unazidi mipaka ya diplomasia ya kawaida. Tuna kila sababu ya kujivunia kuona kwamba uhusiano huu wa kirafiki umekuwa ukidumu na kuimarika siku hadi siku.”
Kubwa zaidi katika maadhimisho ya sherehe hizo ni uzinduzi rasmi wa filamu ya “Amazing Tanzania” ambayo imehusisha marais wawili akiwemo Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania, Dkt: Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa serikali ya mapinduzi ya Zanzibar, Dkt: Hussein Mwinyi pamoja nae msanii mashuhuri wa filamu kutoka nchini China Bwn:Jing Dong .
Waziri Pindi Chana ameongeza kuwa filamu hiyo imelenga kutangaza Tanzania na vivutio vyake katika bara la Asia hususani, soko la kimataifa la China ambalo linazalisha idadi kubwa ya watalii.
“Katika kufanikisha hayo, utangazaji utalii na Utamaduni wa Mtanzania katika masoko mbalimbali ya Kimataifa ikiwemo China ni miongoni mwa mikakati inayoendelea kutekelezwa. Kipekee katika siku hii ya kilele cha maadhimisho ya ushirikiano kati ya Tanzania na China, tutazindua rasmi Filamu ya Amazing Tanzania.
Maandalizi ya filamu hiyo, yamemhusisha Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dkt. Hussen Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi pamoja na Bw. Jing Dong, Msanii Mashuhuri wa filamu kutoka China. Kwa ujumla filamu hii inalenga kutangaza Tanzania na vivutio vyake katika Bara la Asia hususan, soko la Kimataifa la China linalozalisha idadi kubwa ya watalii Duniani.”Alisema Balozi Chana.
Wabobezi wa masuala ya kidiplomasia wanayataja mahusiano hayo kama mahusiano bora zaidi yaliyovuka mipaka ya kidiplomasia hususani katika unufaishaji wa mambo mengi msingi yenye tija zaidi kwa upande wa Tanzania.
Hakika si kazi ndogo iliyofanyika kuleta mageuzi haya nchini pongezi za dhati ziende kwa serikali ya awamu sita ikiongozwa na Rais wake Samia Suluhu Hassan pamoja na wizara ya maliasili na utalii kwa hatua kubwa ya mageuzi katika sekta ya utalii.
Hakika miaka hii 60 kati ya Tanzania na China ni zaidi ya Diplomasia.