Machi 19, mwaka huu, wakati Tanzania ikisogelea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwaka 2015, Uhuru Kenyatta alitangazwa kumshinda Raila Odinga katika kinyang’anyiro cha urais wa Kenya.

Kenyatta, mtoto wa Rais wa Kwanza wa Kenya, Mzee Jomo Kenyatta, alipata kura 6,173,433 akifuatiwa na Odinga aliyepata kura 5,340,546, ikiwa ni tofauti ya kura 832,887 katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Machi 4, mwaka huu.

 

Katika kinyang’anyiro hicho, Musalia Mudavadi alishika nafasi ya tatu baada ya kuvuna kura 483,981, akifuatiwa na Peter Kenneth (72,786), Mohamud Dida (52,848), Martha Karua (43,881) na James ole Kiyiapi (40,998).


Muda mfupi baada ya Kenyatta kutangazwa mshindi, Odinga alipata fursa ya kuwashukuru Wakenya kwa kura alizopata pamoja na mgombea mwenza, Kalonzo Musyoka, lakini akatangaza kutotambua matokeo hayo na kuahidi kwenda kuyapinga mahakamani.

 

Lakini, kikubwa zaidi kilichonisukuma kuandika makala haya ni hatua ya Odinga kuwaasa wafuasi wake kuwa wavumilivu na kutothubutu kufanya fujo, ghasia na uharibifu wa mali.

 

Kwamba wawe watulivu na wavumilivu kusubiri uamuzi wa mahakama, kuhusu kesi atakayofungua dhidi ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IECB) ya Kenya. Lakini pia Odinga alihitimisha hotuba yake fupi kwa kusema, “Mungu Ibariki Kenya.”

 

Hii ni kauli iliyojaa hekima na uzalendo, lakini ambayo inastahili kuigwa na wanasiasa wengine wakiwamo wa hapa Tanzania.


Odinga si tu kwamba amekumbuka madhara makubwa ya vurugu za kisiasa zilizotokea mara baada ya Uchaguzi Mkuu wa Kenya mwaka 2007 uliompeleka Ikulu Mwai Kibaki, lakini pia amejali usalama wa maisha ya Wakenya na mali zao. Anatambua kuwa amani na utulivu ndiyo msingi wa maendeleo katika taifa lolote duniani.


Katika kipindi hiki cha ushindani mkubwa wa kisiasa duniani, wagombea wengi mara baada ya kushindwa wamekuwa wakitoa maneno makali na yenye kila aina ya  uvunjifu wa amani na utulivu. Lakini kwa upande wake, pamoja na hisia za kudhani amedhulumiwa ushindi, Odinga amekataa vurugu. Anapenda kuona usalama na amani vinaendelea kuchanua Kenya.

 

Hapa nimejifunza jambo kutoka kwa Raila Odinga. Kumbe si kweli kwamba wanasiasa wote wanatafuta uongozi kwa ajili ya kujipatia maslahi binafsi na familia zao. Ingekuwa hivyo, mwanasiasa huyo angewasha moto wa ghasia Kenya mara baada ya kutotangazwa mshindi wa urais.

 

Mwanasiasa huyo anaamini (yuko sahihi) kuwa njia sahihi ya kudai haki anayodhani amedhulumiwa ni kutumia chombo cha sheria, yaani mahakama. Ameonesha kuheshimu utawala wa kisheria. Ameahidi pia kuheshimu uamuzi utakaotolewa na chombo hicho cha sheria kuhusu pingamizi lake dhidi ya Kenyatta.


Hapa Tanzania, tayari wanasiasa kadhaa kutoka vyama mbalimbali wameanza kuukodolea macho urais. Wameanza harakati za kuingia Ikulu kupitia Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.


Idadi kubwa ya wanasiasa hawa ni wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Lakini hii haimaanishi kuwa vyama vya Civic United Front (CUF), Tanzania Labour Party (TLP), NCCR-Mageuzi na vinginevyo havina wanachama wanaowania kiti cha urais wa Tanzania kupitia uchaguzi huo.


Watanzania wengi tunapenda kuona wanasiasa wetu wanakuwa mfano mzuri wa kuigwa, katika kuhamasisha na kudumisha amani iliyopo nchini kama alivyofanya Odinga hata baada ya kutopata ushindi aliokuwa anautarajia.


Raila Odinga anapinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliomweka madarakani Uhuru Kenyata, lakini kiukweli hata yeye anajua kuwa katika uchaguzi kuna kushinda na kushindwa, lakini pia asiyekubali kushindwa si mshindani.


Vitu hivi ni muhimu kufahamika kwa wanasiasa wa Tanzania wanaojiandaa kugombea urais, ubunge na udiwani katika Uchaguzi Mkuu ujao.


Niliwahi kuandika katika moja ya makala zangu za uchambuzi, kwamba ukiona mwanasiasa anahamasisha na kuzusha vurugu mara baada ya kubwagwa katika kinyang’anyiro cha wadhifa fulani, basi ujue huyo nia yake haikuwa ya kutafuta uongozi wa kuwatumikia wananchi. Nani anapinga?


Odinga amewaasa wafuasi wake kutothubutu kufanya vurugu baada ya yeye kushindwa na Kenyatta. Lakini ametumia chombo sahihi (mahakama) kupinga matokeo hayo. Huo ni mfano mzuri unaostahili kuigwa na wanasiasa wa hapa Tanzania. Unaposhiriki kugombea nafasi yoyote ya uongozi usisahau dhana ya “asiyekubali kushindwa si mshindani.”


0765 649735