Zaidi ya wafugaji 100 wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha wamenufaika na mafunzo ya ufugaji bora wanyuki, uongezaji thamani mazao ya nyuki, uchakataji wa sumu ya nyuki na uandaaji wa maziwa ya nyuki (Royal Jelly) .

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baada ya Mafunzo hayo yaliyotolewa na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) wafugaji hao wameshukuru kujengewa uwezo wa ufugaji nyuki kisasa 

 “tumejifunza namna sekta hii ya nyuki ilivyo na faida kubwa endapo tutafuga kisasa ikiwa ni pamoja na kuongeza thamani mazao ya nyuki” ameeleza Bw. Meneja Memuruti Menye.

Naye, Mfugaji Bi. Naatosim Parmandi amesema mafunzo ya vitendo yamekua na tija sana, wameweza kutembelea na kushuhudia zoezi la upandishaji na ukaguzi wa mizinga pamoja na uchakataji wa asali unavyofanyika maabara

“kabla ya mafunzo nilikuwa natumia njia za kiasili kuvuna asali ambapo zilikua zikiwaathiri nyuki”. amesema Parmandi

Mtafiti kutoka TAWIRI Bw. Kipemba Ntiniwa ameeleza kuwa, nyuki ni fusra katika kujikomboa kiuchumi ambapo ametoa wito kwa wafugaji waliopata mafunzo kuwa walimu kwa wengine 

“Ili kufuga nyuki kibiashara ni muhimu kujua aina ya nyuki ili kuwa na makundi imara, nitoe wito mkawe walimu wa wengine”. amesema Ntiniwa

Mafunzo hayo yamefanyika Makao Makuu ya TAWIRI Njiro-Arusha ambapo watafiti wa nyuki wametoa elimu ya ufugaji bora wa nyuki wakubwa (wadungao) na nyuki wadogo (wasiodunga), uongezaji thamani mazao yanyuki, utalii wa nyuki, zana za ufugaji nyuki kwa wafugaji.