Na Isri Mohamed

Ikiwa ni miaka takribani 19 na miezi mitano imepita tangu Gwiji wa masumbwi duniani, Mike Tyson (58), atangaze kustaafu ngumi za ushindani, hatimaye ametangaza kurejea katika ngumi za kulipwa na anatarajia kupanda tena ulingoni Novemba 15, 2024 dhidi ya Jake Paul (31), katika ukumbi wa AT&T Stadium mjini Arlington, Texas.

Tyson ambaye Juni 11, 2005, alifikia uamuzi huo baada ya kupoteza pambano lake dhidi ya Kevin McBride kwa ‘TKO’ katika raundi ya sita, lililochezwa kwenye ukumbi wa MCI Center ambao kwa sasa unajulikana kama Capital One Arena.

Tyson na Paul watacheza pambano hilo kwa daraja la uzito wa juu ‘Heavyweight Division fight’ kwa raundi nane zenye dakika mbili, ambapo wote wawili watavaa Gloves za aina ya 14oz kwa ajili ya usalama wao, na sio 10oz ambazo mabondia wa kulipwa huzivaa.

Kwa kuwa ni pambano rasmi la ngumi za kulipwa, ‘Knock Down’ na ‘Knock Out’ zitaruhusiwa, wakati huo huo kikinga kichwa ‘Headgear’ hazitaruhusiwa na matokeo ya pambano hilo yataingizwa katika rekodi rasmi za ngumi za kulipwa Duniani.

Pambano hilo litakuwa la 59 kwa Mike Tyson tangu aanze kucheza ngumi na litakuwa pambano lake la 51 kama atashinda, na ikitokea amepoteza basi atakuwa amepoteza pambano lake la saba.

Kwa upande wa mpinzani wake Jake Paul litakuwa pambano lake la 12, kama atashinda atashinda pambano lake la 11 kama atapoteza atapoteza pambano lake la pili.