Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa serikali itaendelea kuboresha mazingira kwa wawekezaji katika sekta ya kilimo na kuhakikisha kunakuwepo masoko ya uhakika. Haya yatajenga msingi wa kukuza uchumi wa taifa kupitia kilimo.

Akizungumza katika Mjadala wa Kimataifa wa Chakula wa Norman E. Borlaug ulioandaliwa na Taasisi ya World Food Prize Foundation, mjini Des Moines, Iowa, Marekani, Oktoba 31, 2024, Mhe. Rais Samia alisema mkutano huo, ambao hufanyika kila mwaka, unalenga kuwakutanisha wadau wa sekta ya kilimo kama wazalishaji, watafiti, wataalamu wa teknolojia, na wanunuzi wa mazao kutoka nchi mbalimbali.

Rais Dkt. Samia alieleza kuwa ili kufanikisha malengo ya kilimo, ni muhimu kuikaribisha sekta binafsi. Ushiriki wa Tanzania, alisema, unaleta manufaa kwa kuwa kuna mashirika mbalimbali yanayoshughulika na teknolojia, utafiti, ununuzi wa mazao, na uhamasishaji wa uzalishaji na mbinu bora za kilimo.

“Lengo la mkutano ni kuhamasisha nchi kuwa na utoshelevu wa chakula na kuchangia usalama wa chakula duniani. Tumealikwa tuzungumze juu ya juhudi zetu, changamoto tunazokutana nazo, na jinsi tunavyowakaribisha wawekezaji,” alisema Mhe. Rais Samia.

Amehimiza watanzania kuwekeza katika kilimo cha mashamba makubwa kwa kutumia mbinu za kisasa ili kuachana na kilimo cha jadi kinachotumia jembe la mkono.

“Nimefanya ziara kwenye mashamba na viwanda vinavyotumia teknolojia ya kisasa, ikiwa ni pamoja na kilimo cha miwa. Watanzania wanaweza kufuata mfano huo na kufanikisha kilimo cha kisasa,” aliongeza.

Pia, Rais Dkt. Samia aliangazia umuhimu wa kuwa na mfumo wa kodi rafiki na kuhakikisha masoko ya uhakika, pamoja na kuondoa madalali wanaopunguza thamani ya mazao kwa wakulima kwa kununua kwa bei ndogo.