Ujumbe kutoka Benki ya Dunia umeonesha kuridhishwa na utekelezaji wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) unaoendelea Chuo Kikuu Mzumbe, baada ya kufanya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa majengo mapya ya taaluma. Mradi huu unalenga kuboresha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia.

Akizungumza katika ziara hiyo ya siku moja, iliyojumuisha wataalam kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha, amesema ujenzi wa majengo mapya ya taaluma unagharimu shilingi bilioni 13.2, fedha zilizotolewa na Benki ya Dunia.

Kiongozi wa timu ya Benki ya Dunia, Prof. Roberta Malee, ameutaka uongozi wa Chuo Kikuu Mzumbe kuhakikisha ujenzi huo unazingatia viwango vya juu vya ubora ili kunufaisha vizazi vya sasa na vijavyo. Pia ameipongeza menejimenti ya chuo kwa usimamizi mzuri wa mradi huo hadi kufikia hatua za sasa.

Dkt. Kennedy Hosea, mratibu wa mradi wa HEET nchini Tanzania, amesisitiza umuhimu wa kukamilisha mradi kwa wakati, akieleza kuwa ni hatua muhimu katika kuboresha mfumo wa elimu ya juu nchini. “Mradi huu unalenga kutoa fursa za kujifunza zinazokidhi mahitaji ya soko la ajira,” alisema Dkt. Hosea.

Msanifu wa majengo, Bw. Fadhili Msemo, amesema majengo hayo yatakuwa na madarasa ya kisasa, maabara, na maeneo maalum kwa tafiti za TEHAMA, hali itakayoongeza ubora wa maendeleo ya kitaaluma na kiteknolojia kwa wanafunzi na wahadhiri wa Chuo Kikuu Mzumbe.

Kampuni ya Shanxi Construction Investment Group kutoka China ndiyo inayoongoza ujenzi wa majengo hayo, baada ya kusaini mkataba wa ujenzi wa miezi 18 mwezi Agosti mwaka huu.