Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

JUMLA ya watoto 85 wamezaliwa kwa huduma ya kupandikiza mimba inayotolewa na kituo cha Kairuki Green IVF tangu kuanzishwa kwake mwaka 2022.

Hayo yalisemwa jana Bunju Mianzini jijini Dar es Salaam kilipo kituo hicho na Mkurugenzi wa Kituo hicho, Dk. Clementina Kairuki, wakati mke wa Rais wa Zambia, Monica Chakwera alipotembelea kituo hicho.

Alisema huduma hiyo imeonyesha mafanikio makubwa tangu kuanzishwa kwake na kwamba mpaka kufikia mwishoni mwa mwaka huu wanatarajia kufikisha watoto 100.

Alisema ndani ya muda mfupi wamefanikiwa kutambuliwa kimataifa kwa kupata ithibati ya ubora (ISO) na kwamba wamefanikiwa kupata wateja kutoka Congo DRC, Comoro, Marekani, Uingereza, Sweeden na mataifa mbalimbali ambao wamepata watoto na wanaendelea vizuri.

Alisema ingawa kiwango cha mafanikio ya tiba hiyo kidunia (success rate) huwa ni asilimia 45 mpaka 50 lakini Kairuki IVF imeweza kufikisha mafanikio ya kupata watoto kwa njia ya upandikizaji na kufikia wastani wa asilimia 63.

Naye Mke wa Rais wa Malawi, Monica Chakwera alielezea kufurahishwa kwake na huduma za upandikaji mimba inazotolewa na Kituo cha Kairuki IVF na kusema kuwa anatamani kuona huduma kama hizo zinaanza kutolewa nchini mwake.

Picha mbalimbali ziara ya mke wa Rais wa Malawi, Monica Chakwera katika kituo cha kupandikiza mimba cha Kairuki Green IVF Bunju Mianzini Dar es Salaam

Alisema kituo cha Kairuki IVF kimekuwa msaada kwa wanawake wengi ambao wameshindwa kupata ujauzito kwa njia ya kawaida hivyo upandikizaji umekuwa ukirudisha furaha kwa wanawake hao.

“Nimeambiwa kwamba tangu kianzishwe mwaka 2022 watoto 85 wameshapatikana kwa njia ya upandikizaji mimba. Hii ni taarifa njema sana kwani watu wengi walihangaika kupata huduma kama hizi Ulaya na mataifa yaliyondelea lakini sasa zinapatikana kwenye nchi zetu ni jambo la fahari sana,” alisema

“ Sijawahi kusikia kituo kama hiki kwetu Malawi lakini ningependa kuona kinaanzishwa ili kuwapunguzia gharama watu wetu wanaolazimika kusafiri kwenda mataifa yaliyoendela kutafuta huduma kama hizi za upandikizanji mimba,” alisema

Alisema anatarajia kufanya harambee kwaajili ya kupata kiasi kikubwa cha fedha zitakazotumika kuwasaidia wanawake wenye shida ya kupata watoto kutumia njia hiyo kumaliza shida zao.

Mkurugenzi wa hospitali ya Kairuki, Asser Mchomvu alisema walipata wazo la kuanzisha kituo hicho baada ya kupata watu wengi wenye shida ya kupata ujauzito waliokuwa wanafika hospitali ya Kairuki Mikocheni wakitafuta huduma hiyo.

Alisema wanawake wengi wamekuwa wakiteseka kwenye ndoa zao kwa kushambuliwa na ndugu jamaa na marafiki inapotokea hajapata ujauzito wakati tatizo linaweza kuwa ni mbegu hafifu za mwanaume.

“Kwa tamaduni za makabila mengi Afrika mtoto asipopatikana basi wanawake wamekuwa wakionekana kuwa ndiyo wenye matatizo lakini kwa uhalisia wakienda kupima wanaume wengi wanakutwa na tatizo hilo kwa hiyo sisi tuliliona tukaona tukaona tuanzishe kituo kumaliza tatizo hilo watu wapate watoto waishi kwa furaha,” alisema