Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Malinyi

MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi wametakiwa kuwa mfano katika kutoa hamasa kwa wananchi kushiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika tarehe 27 Novemba 2024.


Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Malinyi, Saida Mhanga wakati akitoa neno la serikali kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Malinyi, Sebastian Waryuba katika Kikao cha Baraza la Madiwani lililofanyika tarehe 30 Oktoba mwaka huu kwa ajili ya kujadali taarifa za utekelezaji robo ya kwanza Julai – Septemba, 2024.

Mkurugenzi wa Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi, Khamis Katimba akizungumza wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani tarehe 30 Oktoba 2024.


Pia aliwataka viongozi na timu ya wataalamu kutoka halmashauri kuhakikisha miradi yote ya serikali inayotekelezwa Malinyi, inatekelezwa kwa wakati na kwa ubora.
“Miradi yote ya serikali itekelezwe kwa wakati na iendane na thamani ya pesa amabazo serikali inagharamia ili kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi,” alisema.


Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi, Pius Mwelase ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Ngoheranga, aliwaomba madiwani kusimamia makusanyo ya mapato katika maeneo yao ili halmashauri iweze kukamilisha miradi iliyokusudiwa kutekelezwa kwa mwaka 2024/2025.


Mwelase alisema, mara baada ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kumalizika, halmashauri inatarajia kuendesha semina elekezi kwa watendaji ngazi ya vijiji ili kuwajengea uwezo katika kutekeleza majukumu yao kikamilifu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi, Khamis Katimba alisema, halmashauri hiyo inatarajia ifikapo Oktoba 2024 kukusanya asilimia 60.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi, Pius Mwelae akizungumza wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani tarehe 30 Oktoba 2024.


Na kwamba, asilimia 40 ya makusanyo hayo yanatarajiwa kupelekwa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.


Sambamba na hilo Katimba aliwashukuru wajumbe wa Baraza la Madiwani kwa kuzingatia mafunzo ya Utawala Bora aliyoyatoa Septemba mwaka huu, ambapo yamewezesha kikao cha baraza hilo kwa mara ya kwanza kufanyika chini ya dakika 30


Mjumbe wa Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Itete, Anatory Libawa alisema, madiwani kwa pamoja wamekubaliana kupunguza ushuru wa pumba kutoka Tsh. 1500 hadi Tsh 500.


Alisema, lengo ni kutoa nafasi kwa wafanyabiashara kutoka maeneo mbalimbali mwenda Malinyi kununua pumba kwa wingi.

Baadhi ya madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro wakiwa katika Kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika tarehe 30 Oktoba 2024.