Bondia Hassan Mwakinyo ametangaza ujio wa pambano lake Novemba 16, mwaka huu la kutetea mkanda wa Afrika wa WBO huku akitamba kuwa yuko tayari kumlaza mtoto wa mtu chini.

Mwakinyo licha ya kutangaza ujio huo hajaweka hadharani mpinzani wake lakini akionekana kutupa vijembe kwa mpinzani wake Twaha Kassim ‘Kiduku’ kuonesha wazi anatamani kupigana naye.

Akizungumza Dar es Salaam kuhusu pambano hilo lijalo, Mwakinyo amesema anaamini katika uwezo wake, makocha wake na timu yake na yuko tayari kwa vita.

“Nina hamu ya kuonesha Watanzania kwamba bado nipo, nilikuwa nina hamu kwa kipindi kirefu kupata nafasi ya kuonesha Tanzania mimi ni nani katika ngumi, nafahamu kurudi kwangu kunaweza kuwa habari njema kwa watu au habari mbaya ila nitapigana,”amesema.

Mwakinyo amesema anaendelea kufanya mazoezi kujiweka tayari kwa pambano hilo ambalo mashabiki wengi wanatamani kujua mpinzani wake ajaye.

Bondia huyo mwenye nyota tatu na nusu mara ya mwisho kuchukua mkanda huo wa WBO Afrika ni Juni 24, mwaka huu Dar es Salaam baada ya kumchapa Patrick Allotey wa Ghana.