Na Mwandishi Wetu, Mwanza
Serikali ya Tanzania imewekeza Sh60 bilioni kuboresha bandari tatu kuu za Ziwa Victoria.
Meneja wa Bandari za Ziwa Victoria, Erasto Lugenge aliwaambia wandishi wa habari waliotembelea bandari za Bukoba na Kemondo kuwa uwekezaji huu mkubwa katika bandari za Kemondo, Bukoba na Mwanza Kaskazini unatarajiwa kuboresha ufanisi na uwezo wa huduma za usafiri katika eneo hilo.
Bw. Lugenge, ambaye anasimamia bandari 12 upande wa Tanzania wa ziwa hilo, amesema kuwa kazi inaendelea vizuri, huku Bandari ya Kemondo ikiwa karibu kukamilika.
“Kazi ya kuboresha Bandari ya Kemondo, ambayo imepewa uwekezaji wa Sh20.339 bilioni, imekamilika kwa asilimia 98,” alisema, akiongeza kuwa hatua za mwisho zinahusisha kusafisha eneo kabla ya kuzinduliwa rasmi.
Mradi wa kuboresha Bandari ya Bukoba kwa Sh19.544 bilioni umefikia asilimia 75 ya kukamilika.
“Kwa mujibu wa makubaliano, miradi hii ilikuwa imepangwa kukamilika ndani ya miezi 18, ikitarajiwa kukamilika tarehe 4 Novemba 2024. Kwa kuwa kazi nyingi tayari imefanyika, sasa ni juu ya mkandarasi na mhandisi mshauri kutathmini kama itakamilika kwa wakati au kama itahitajika muda mfupi kidogo ili kumaizia,” Bw Lugenge alisema.
Miongoni mwa bandari 12 anazosimamia Bw. Lugenge, sita ni vituo vikuu, vikiwemo Mwanza Kaskazini, Mwanza Kusini, Bukoba, Kemondo, Nansio-Ukerewe, na Musoma. Maboresho yanayoendelea yanakusudia kuongeza kina cha maji kutoka mita 3.5 hadi mita 5 katika Bandari za Kemondo na Bukoba. Pia, mabadiliko mengine yanahusisha kuongeza urefu wa gati kutoka mita 75 hadi 92, kuboresha eneo la sakafu kwa kuimarisha muundo wa zege, na kufunga uzio wa kuimarisha usalama.
Maboresho mengine yanajumuisha ujenzi wa maeneo ya kusubiri abiria, vituo vya ukaguzi wa mizigo, mfumo wa umeme wa kisasa, na kinga ya upepo.
“Tunaanzisha vituo vya huduma vya sehemu moja katika bandari zote zinazoboreshwa, tukijumuisha huduma za Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Misitu, Uhamiaji, Afya, na Wakala wa Forodha na Uondoshaji Mizigo pamoja na vikosi vya ulinzi na usalama ili kuboresha utoaji wa huduma,” Bw Lugenge alieleza.
Maboresho haya yanalenga kusaidia kupokea MV Mwanza Hapa Kazi Tu, meli mpya ya abiria inayojengwa na ambayo itakuwa kubwa zaidi Afrika Mashariki. MV Mwanza Hapa Kazi Tu itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 1,200, tani 400 za mizigo, magari madogo 20, na magari makubwa matatu, hivyo kuongeza maradufu uwezo wa abiria ikilinganishwa na MV Victoria inayobeba abiria 600 kwa sasa.
Meli hiyo inatarajiwa kuanza shughuli zake Desemba 2024 au Januari 2025, na maboresho ya bandari yanapiga hatua ili kukidhi muda wa uzinduzi. “Tunatarajia kuwa MV Mwanza Hapa Kazi Tu itaanza kufanya kazi mwishoni mwa mwaka au mwanzoni mwa mwaka ujao, hatua ambayo italeta maboresho makubwa katika huduma za usafiri kwenye Ziwa Victoria,” Bw Lugenge alithibitisha.
Uwekezaji wa serikali na kukamilika kwa maboresho haya ya bandari yanatarajiwa kurahisisha safari na kuongeza shughuli za kiuchumi katika eneo hilo, na kuweka viwango vipya kwa huduma za usafiri wa ziwani kote Afrika Mashariki.
Tayari nchi za Burundi, DRC na Rwanda zimeonyesha nia ya kutumia bandari hizo zitakapokamilika.
Hili litawezekana kutokana na uwepo wa huduma ya reli ya kisasa ya SGR na reli ya MGR, zinazounganisha Jiji la Dar es Salaam na Ziwa Victoria kupitia Mwanza.