Hezbollah imetangaza kuwa naibu katibu mkuu wa kundi hilo atakuwa mkuu wake mpya.
Naim Qassem anachukua nafasi ya kiongozi wa muda mrefu Hassan Nasrallah, ambaye aliuawa katika shambulio la anga la Israel huko Beirut mwezi uliopita.
Ni mmoja wa viongozi wachache waandamizi wa Hezbollah ambao wamesalia hai, baada ya Israel kuua viongozi wengi wa kundi hilo katika mfululizo wa mashambulizi.
Uteuzi huo unafanyika huku mzozo nchini Lebanon ukiendelea kuongezeka katika wiki za hivi karibuni.
Kwa zaidi ya miaka 30, Naim Qassem alikuwa naibu katibu mkuu wa Hezbollah na mmoja wa watu wanaotambulika zaidi katika kundi hilo.
Hezbollah ilisema alichaguliwa na Baraza la Shura, kwa mujibu wa kanuni za kundi hilo.
Hata hivyo, hajulikani mahali alipo huku baadhi ya ripoti zikionyesha kuwa amekimbilia Iran, ambayo ni mfuasi mkubwa wa Hezbollah.
Ikitangaza kupandishwa cheo kwa Qassem, Hezbollah ilitoa taarifa ikimuelezea kama “aliyebeba bendera iliyobarikiwa”.
Taarifa hiyo pia ilimheshimu marehemu Nasrallah na wengine waliouawa katika vita hivyo.
Uongozi mpya wa Hezbollah ulitarajiwa kupitishwa kwa Hashem Safieddine, lakini tarehe 22 Oktoba ilifichuliwa kwamba aliuawa katika shambulio la anga la Israel karibu wiki tatu kabla.