Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
JUMLA ya watahiniwa 974,229 kati ya 1,204,899 waliofanya mtihani ambao ni
sawa na asilimia 80.87 ya watahiniwa wenye matokeo wamefaulu mtihani wa kumaliza Elimu ya Msingi 2024.
Aidha Baraza la Mitihani Tanzania limefuta matokeo yote kwa jumla ya watahiniwa 61 ambao walibainika kufanya udanganyifu na kuandika lugha ya matusi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 29, 2024, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania, Dkt. Said Mohamed amesema mwaka 2023 watahiniwa waliofaulu walikuwa asilimia 80.58 hivyo ufaulu umeongezeka kwa asilimia 0.29.
Amefafanua kuwa, kati ya watahiniwa 974,229 waliofaulu, wavulana ni 449,057 sawa na asilimia 81.85 na wasichana ni 525,172 sawa na asilimia 80.05.
“Mwaka 2023 wasichana waliofaulu walikuwa asilimia 80.58 na wavulana walikuwa asilimia 80.59. Hivyo, ufaulu wa wasichana umeshuka kwa asilimia 0.53 na ufaulu wa wavulana umeongezeka kwa asilimia 1.26,” amesema.
Amesema ubora wa ufaulu kwa watahiniwa waliopata madaraja ya A na B umeimarika ambapo watahiniwa 431,689 sawa na asilimia 35.83 wamepata madaraja ya A na B ikiwa ni ongezeko la asilimia 8.65 ikilinganishwa na mwaka 2023.
Ameongeza kuwa kati ya watahiniwa 431,689 waliopata madaraja A na B, wasichana ni 216,568 (33.01%) wakiwa na ongezeko la asilimia 9.09 na wavulana ni 215,121 (39.21%) wakiwa na ongezeko la asilimia 8.28 ikilinganishwa na mwaka 2023.
Akizungumzia kuhusu waliofutiwa matokeo amesema, watahiniwa 45 ambao walibainika kufanya udanganyifu katika mtihani wamewafutiwa kwa mujibu wa Kifungu cha 5(2)(j) cha Sheria cha Baraza la Mitihani Sura ya 107 kikisomwa pamoja na Kifungu 30(2)(b) cha Kanuni za Mitihani za Mwaka 2016.
“Watahiniwa 16 waliandika lugha ya matusi katika Skripti zao kwa mujibu wa Kifungu cha 17(1) cha Kanuni za Mitihani za Mwaka 2016,” amesema.
Pia Baraza hilo limezuia kutoa matokeo ya watahiniwa 418 ambao waliugua au kupata matatizo mbalimbali na kushindwa kufanya Mtihani kwa idadi kubwa ya masomo au masomo yote.
“Watahiniwa husika wamepewa fursa ya kurudia kufanya Mtihani wa kumaliza Elimu ya Msingi (PSLE) mwaka 2025 iwa mujibu wa Kifungu cha 32(1) cha Kanuni za Mitihani,” amesema.