Usafiri Dar ni zaidi ya kero
Jiji la Dar es Salaam linakabiliwa na changamoto nyingi, lakini kubwa kuliko zote imejikita katika usafiri wa kutumia magari.
Kero ya usafiri inachangia kwa kiwango kikubwa kuathiri ratiba na hata uchumi kwa wakazi wa Dar es Salaam. Kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele, ndivyo usafiri unavyozidi kuwa wa shida katika jiji hili. Wengine wanaliita Jiji la Raha na Karaha. Bila kujali aina ya usafiri unaotumia – iwe unatumia gari binafsi, au la umma, usafiri jijini Dar es Salaam ni zaidi ya kero.
Hali ni mbaya zaidi katika vituo vya daladala. Huwezi kuingia garini kama hauna ubavu wa kupambana, kusukumana na wakati mwingine kupigana viwiko na wasafiri wengine. Kuingia kupitia dirishani pia si kitendo cha ajabu Dar es Salaam.
Ukikosa uwezo wa kukabili hali hiyo, basi uwe tayari kusubiri karibu siku nzima kituoni, lakini pia kufuta ratiba ulizojipangia siku hiyo. Hii ndiyo Dar es Salaam, ukipenda unaweza kuiita Dar, au Bongo.
Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari nao hutaabika zaidi na aina hii ya usafiri. Wengi wao hawana uwezo wa kumudu mapambano hayo. Wanafika shuleni wakiwa wameshachoka, achilia mbali kuchelewa vipindi vya masomo darasani.
Taswira ya aina hii inaweza kuchangia wanafunzi hawa kutofanya vizuri katika mitihani yao. Katika nchi nyingine serikali imetenga magari maalumu kwa ajili ya kusafirisha wanafunzi.
Ukifika katikati ya Dar kwa mara ya kwanza, unaweza kuamini kuwa magari ni mengi kuliko binadamu wanaoishi katika jiji hili. Misururu ya magari inaonekana barabarani saa 24. Ingawa sina ushahidi wa moja kwa moja, lakini naweza kuamini kuwa daladala za Dar es Salaam zinazeeka kabla ya muda wake uliokadiriwa kutoka kiwandani.
Kwanini nadhani sikosei kusema hivyo? Daladala za Bongo zinapakia abiria wengi kupindukia. Mara nyingi wanaosimama ndiyo wengi kuliko wanaoketi vitini. Utaratibu huu hauwezi kuiacha gari salama kwa muda mrefu.
Msongamano wa abiria kwenye daladala ni sawa na kusema tisa; kumi ni adha ya kusubiri barabarani. Kuna wakati katika barabara nyingi zikiwamo za Morogoro, Ali Hassan Mwinyi, Mandela, Chang’ombe na Shekilango magari husimama kwa zaidi ya nusu saa kungoja nafasi ya kusogea mbele.
Wakati huo karibu abiria wote waliosongamana ndani ya daladala huvuja jasho la nguvu, na huo ndiyo mwanya wa kuambukizana magonjwa ya ngozi na kadhalika. Angalau wanaotumia usafiri binafsi wakati mwingine hujikuta wamefaidi kausingizi.
Tatizo hili la msongamano wa magari barabarani linachangiwa na ufinyu wa barabara, ukorofi wa madereva wachache na baadhi ya askari wa usalama barabarani (trafiki) kukosa ubunifu na umakini katika kuongoza magari.
Kero hii huyalazimu magari kutumia saa nyingi kusafiri umbali mfupi. Hata viongozi wakuu wanaonja adha hii ya usafiri kwa kusubiri kwanza trafiki wazuie magari waweze kupita.
Usafiri Dar es Salaam umeendelea kuwa kero isiyomithilika hata baada ya ‘Treni ya Mwakyembe’ kuanza kutoa huduma ya kusafirisha abiria jijini.
Idadi ya wanaolazimika kusimama ndani ya usafiri huu ni kubwa kuliko wanaobahatika kukaa vitini. Unafuu pekee wa gari moshi hili ni kwamba halina ‘mpinzani’ relini, linawahi kukamilisha safari zake.
Kifanyike nini sasa kupunguza kero ya usafiri Dar es Salaam? Fikra ya Hekima inaikumbusha Serikali kuweka mipango mikakati ya kisayansi kukabili tatizo hili.
Ipanue barabara zilizopo na kujenga za juu (flyovers). Iongeze treni na mabehewa, iongeze trafiki barabarani na kujenga mazingira yatakayowezesha uwekezaji zaidi katika biashara ya usafirishaji wa abiria jijini.
Bongo isiyo na kero ya usafiri wa kutumia magari inawezekana.