Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani
Baada ya Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, kukamilisha ziara maalum mkoani amechukua hatua ya haraka kwa kumpigia simu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi Eng. Aisha Amour, pamoja na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Lazaro Kilahala, na kuwaagiza wafike Mafia mara moja na kupiga kambi hadi huduma ya kivuko irejee.
“Msiondoke Mafia mpaka kivuko kianze kutoa huduma kwa wananchi,” Waziri Bashungwa alisisitiza,
Alieleza, Serikali imedhamiria kutatua changamoto za usafiri katika kisiwa hicho.
Alieleza kuwa, kutokana na gharama kubwa ya usafiri wa ndege, usafiri wa kivuko unabaki kuwa chaguo kuu kwa wakazi wengi wa Mafia, suala ambalo linaumiza.
Bashungwa aliongeza kuwa serikali, kwa kushirikiana na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, inaendelea na ukarabati wa Meli ya TNS Songosongo ili kutoa huduma mbadala kwa wananchi wa Mafia wakati kivuko cha MV Kilindoni kikiwa kwenye matengenezo.
Pia, alieleza kuwa serikali imetenga zaidi ya sh.Bilioni 9 kwa ajili ya ujenzi wa kivuko kipya kitakachosaidia kuboresha usafiri kati ya Mafia na Nyamisati, na kuongeza idadi ya vivuko kuwa vitatu.
Baadhi ya wakazi wa Kata ya Kilindoni, Mafia, walitoa kilio chao kuhusu kukosekana kwa huduma ya usafiri wa kivuko, hali inayowalazimu kutumia vyombo visivyo salama kama mashua, na kuathiri usafirishaji wa bidhaa na huduma muhimu.
Adam Swed na Sajida Ismail, wakazi wa Kilindoni, walisema kuwa usafiri wa ndege ndiyo chaguo pekee la uhakika kwa sasa, ingawa wengi wao hawana uwezo wa kumudu gharama za usafiri wa anga.
Waliiomba serikali kuendelea kusimamia na kutatua kero ya usafiri wa kivuko, wakieleza kuwa hali hiyo imeongeza gharama za maisha na kuathiri upatikanaji wa huduma nyingine za kijamii.