Iran imemnyonga mpinzani wa Ujerumani na Iran Jamshid Sharmahd, baada ya kukutwa na hatia ya “kuongoza operesheni za kigaidi”, vyombo vya habari vya serikali vinaripoti.
Sharmahd alihukumiwa kifo mwaka jana baada ya kushutumiwa kwa kuongoza kundi la wafuasi wa kifalme lenye makao yake makuu nchini Marekani.
Alikuwa amekanusha mashtaka, huku familia yake ikisema kuwa yeye ni msemaji tu. Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani alisema Berlin imeonya mara kwa mara Tehran kuwa kunyongwa kwa raia wa Ujerumani “kutakuwa na madhara makubwa”.
“Kuuawa kwa Jamshid Sharmahd kunaonesha ni aina gani ya sheria za utawala zisizo za kibinadamu (nchini Iran),” Annalena Baerbock alichapisha kwenye X.
Mashirika ya haki za binadamu yamelaani kunyongwa kwa Sharmahd, ambaye aliishi Marekani.
“Mchakato mzima, ikiwa ni pamoja na kukamatwa kwake, kuhukumiwa, na kunyongwa, ni ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa,” alisema Mahmood Amiry-Moghaddam, mkurugenzi wa kundi la Haki za Kibinadamu la Iran lenye makao yake makuu nchini Norway.