Na Lusungu Helela, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George  Simbachawene ameonesha kukerwa na  baadhi ya Wakurugenzi na Wakuu wa Taasisi za Serikali  wenye  tabia ya kuwafokea Watumishi  walio chini yao  wakiamini kufanya hivyo ndio uongozi.

Amesema baadhi yao hudiriki hata kuwatukana watumishi huku akisisitiza jambo hilo ni kosa kubwa na kama kuna kiongozi anataka kufanya ufanisi lakini anafikia hatua ya kutukana watumishi huyo hafai kabisa kwani zipo kanuni, taratibu na sheria za utumishi wa umma za kuchukua kama mambo hayaendi sawa

Ametoa kauli hiyo leo wakati alipokuwa akizungumza na Watumishi wa Chuo cha Utumishi wa Umma katika Kampasi ya Dar es Salaam ambapo amesema hivi vitu ni maslahi ya umma, Kiongozi makini hahitaji kununa wala kufokafoka cha msingi ni kuchukua hatua.

” Kuna watu walikuwa wanasoma  bidii zote ili wapate nafasi kwenye utumishi wa umma ili waje wakomeshe watu, kuna watu kazi yao kubwa ni kuwashughulikia watu na hiyo ndo raha yao” ameng’aka Simbachawene

Amesema mshahara hata uwe mkubwa kiasi gani kwa watumishi kama mahali hapo  pa kazi hakuna amani, kuna manyanyaso, hakuna kuthaminiwa na kutambuliwa kwa mchango wao hapawezi kuwa na ufanisi wa kazi.

Kufuatia hatua hiyo, Mhe.Simbachawene amesema akitaka Chuo Cha Utumishi wa Umma kisisubiri kuitwa kitoe mafunzo ya kujengeana uwezo mahali pa kazi pamoja na kuhakikisha  kinatoa mafunzo ya awali kwa watumishi wanapoanza kazi  ili waweze kutambua haki na wajibu wao.

Amesema huko kwenye Taasisi za Serikali kuna shida kubwa ya migogoro ya watumishi isiyoisha ilhali Chuo cha Utumishi kipo ” nilitegemea kuona mnafika kwenye Taasisi hizo  kwa lengo la kutoa mafunzo kwa watumishi ili mambo yaende lakini hamfanyi hivyo”

” Nakutana na mashirika makubwa ya nje yananiomba yakatoe mafunzo ya kuwajengea uwezo katika Taasisi fulani za Serikali wanaona mambo hayaendi sawa ilhali ninyi mpo hii sio sawa  changamkeni mna fursa nyingi za kubadilisha utumishi wa  umma nchini.

Amesema Chuo hicho kifanye mafunzo ili kuepuka watumishi wengi kupelekana mahakamani au TAKUKURU ilhali Chuo cha Utumishi kupitia mafunzo ya kujengeana yangetolewa ingekuwa ni mwarobaini na  hali  isingefikia huko.

Awali Mkuu wa Chuo hicho, Dkt.Mabonesho ameishukuru Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa mchango  mkubwa wa kutatua tatizo la watumishi katika Chuo ambacho kilikuwa kinakabiliwa na uhaba wa watumishi na hivyo kukwamisha kufikia malengo waliyojiwekea.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George  Simbachawene akizungummza na  Watumishi wa Chuo cha Utumishi wa Umma  Kampasi ya Dar es Salaam.

Baadhi ya Watumishi wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George  Simbachawene wakati alipofanya ziara ya kutembelea Chuo cha Utumishi wa Umma  Kampasi ya Dar es Salaam.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George  Simbachawene akipata maelezo wakati alipotembelea chumba cha  mashine za kizamani za kujifunzia za  kuchapa kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza  katika Chuo cha Utumishi Kampusi ya Dar es Salaam akiwa na Mkuu wa Chuo hicho Dkt. Ernest Mabonesho.

Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma, Dkt. Ernest Mabonesho akizungumza kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George  Simbachawene kwa ajili ya kuzungummza na  Watumishi wa Chuo hocho  Kampasi ya Dar es Salaam 

Kwaya ya Chuo cha Utumishi wa Umma ikiimba mbele ya  Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George  Simbachawene wakati alipowasili  katika  Chuo hicho kwa ajili ya kuzungumza na Watumishi.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George  Simbachawene akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya  Watumishi wa Chuo cha Utumishi wa Umma