Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
CHAMA cha Waandishi wa habari Wanawake Tanzania (TAMWA) na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) wameongeza muda wa maombi ya ushiriki katika Tuzo za Samia Kalamu Awards hadi Oktoba 30, 2024.
Tuzo hizo zitatolewa kwa wanahabari wa kitanzania zikiwa na lengo la kuhamasisha, kukuza na kupanua wigo wa uandishi, utangazaji na uchapishaji wa maudhui ya ndani, kupitia vyombo vya habari vya asili na mitandaoni, ili kuchochea uandishi wa makala za kina zinazozingatia maendeleo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 24, 2024, Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa Dkt. Rose Reuben amesema awali tarehe ya mwisho ya kuwasilisha maombi ilikuwa Oktoba 26, mwaka huu.
“Uamuzi wa kuongeza muda umefanyika ili kutoa nafasi zaidi kwa wale waliokutana na changamoto za kiufundi, ikiwamo kushindwa kupandisha kazi mitandaoni na changamoto nyingine.
“tunapenda kuwakumbusha kuwa kazi zinazowasilishwa zinatakiwa kuwa za kipekee na ambazo hazijawahi kuwasilishwa kuwania tuzo nyingine, na zinazofuata taratibu za haki miliki. Waandishi wanatakiwa kuwasilisha kazi zao kupitia tovuti rasmi ya www.samiaawards.tz,”amesema Dk.Rose.
Amesema hiyo fursa adhimu kwa vyombo vya habari, waandishi wa habari, na maafisa bari kuonesha umahiri wao wa kuchakata habari na kuthaminiwa kwa michango katika taaluma ya uandishi.
Amebainisha kuwa, hadi Oktoba 23, mwaka huu wamepokea maombi kutoka mikoa 23 ya Tanzania ikiwemo Dar es Salaam, Dodoma, Shinyanga, Mwanza, Mtwara, Simiyu, Geita, Njombe, Mbeya, Songwe,Rukwa, Katavi, Kigoma, Tabora, Kagera, Mjini Magharibi, Ruvuma, Lindi, Kilimanjaro, Manyara, Morogoro na Pwani.
“Tunawahimiza wanahabari kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhim wa kushiriki katika upigaji kura kwa wingi, kwani kura za wananchi zinachangia asilimia 60 ya alama za mshindi, huku asilimia 40 zikiamuliwa na jopo la majaji. Wananchi wataweza kupiga kura kupitia namba maalumu ya SMS SHORT CODE 15200 au kwa kutumia tovuti rasmi,”ameswma Dk.Rose.
Naye Meneja wa Huduma za Utangazaji wa TCRA,Mhandisi Andrew Kisaka amesema tuzo hizo ni muhimu kwa ajili ya kukuza na kutambua mchango wa waandishi wa habari katika masuala mbalimbali yakiwemo ya maendeleo.
“Tunaamini mna michango mizuri kwa jamii kupitia kazi zenu mlizozifanya kwenye redio, televisheni na mitandao ya kijamii. Nawahimiza kuziwasilisha kwa haraka katika kipindi hiki kilichobaki kwani tunaamini zimeleta mabadiliko chanya kwenye jamii,”amesema Mhandisi Kisaka.