*Yazindua maabara ya kisasa kwa fedha za wanakijiji
*Tume yaguswa, kuhamishia hamasa shule 4,000 za Kata

Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Moshi

SHULE ya Sekondari ya Manushi iliyopo Kata ya Kibosho Magharibi wilayani Moshi, Kilimanjaro imeandika historia ya kuwa shule ya kwanza ya aina hiyo kujenga maabara yake ya kisasa ya TEHAMA.

Kwa ujenzi wa maabara hiyo, shule sasa ina uhakika wa kuwapika vijana wake kwa elimu ya kisasa, kutokana na maabara hiyo kusheheni vitabu vyote vya ziada na kiada, hivyo kuondokana na changamoto za upatikanaji wa vitabu kama ilivyo kwa shule nyingine zilizopo pembezoni.

Uzinduzi huo ulifanywa na mgeni rasmi, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Nkundwe Mwasaga hivi karibuni kijijini Manushi wakati wa hafla hiyo iliyokwenda sambamba na mahafali ya 15 ya shule.

“Nina furaha kubwa sana kualikwa hapa Manushi. Hapa panakwenda kuandika historia kubwa katika mapinduzi ya kidigitali. Tumezoea kuona maendeleo ya Tehama yakionekana mijini zaidi, lakini sasa tunakwenda kugeukia kila kona ya nchi ili uchumi wa kidigitali umfikie kila Mtanzania, mpaka wa kijijini.

“Kama kituo, sisi Tume tutahakikisha mafunzo mbalimbali yanatolewa ili vijana hawa wa Manushi wawe mahiri katika TEHAMA. Wawe chachu ya wananchi wa Manushi na mkoa wa Kilimanjaro kukimbilia TEHAMA kama ambavyo tunadhamiria hiki kitu kisambae kwa kila Mtanzania,” alisema.

Aliongeza kuwa, historia iliyoandikwa ya uzinduzi wa maabara ya kisasa ya TEHAMA kijijini itakwenda kuziamsha shule nyingine zaidi ya 4,000 za Kata nchini, jambo ambalo litakwenda kupunguza kwa kiasi kikubwa ubora wa elimu katika ya shule za mijini na vijijini.

“Ndiko tunakoelekea. Leo Manushi wanakwenda kupika wataalamu. Na ni hawa hawa wanaokwenda kuwa kioo na kichocheo cha kusambaa kwa kasi elimu ya Tehama kama nyenzo ya kuchochea mapinduzi makubwa sana ya TEHAMA kuelekea katika uchumi wa kidigitali.

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Nkundwe Mwasaga (katikati) akishuhudia wanafunzi wakiwa katika darasa la kisasa la TEHAMA katika Shule ya Sekondari ya Manushi lililozinduliwa hivi karibuni kijijini Manushi, wilayani Moshi, Kilimanjaro

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya TEHAMA, Profesa Leonard Mselle ambaye amekuwa mstari wa mbele kuhamasisha ujenzi wa maabara na maendeleo ya shule hiyo, aliwashukuru wana-Manushi kwa michango na kwamba wasichoke kuchangia shughuli nyingine za maendeleo, akitolea mfano ujenzi wa mabweni na bwalo la chakula, miradi inayokusudiwa kuanzishwa hivi karibuni.

Mkuu wa Shule, Hamisi Mbawa alisema uwepo wa mradi huo utarahisisha shughuli nzima ya utoaji elimu kwa haraka na kwa ufanisi mkubwa.

Aliongeza kuwa, ana uhakika mradi huo uliogharimu Sh milioni 52 utasaidia wanafunzi kupata uelewa na ujuzi wa TEHAMA na kwamba vifaa vya kisasa vitachangia uelewa katika masomo na namna ya kukabiliana na maisha bora ya kisasa.

Naye Mhandisi Bahanza Amali, Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya QSoft Technology iliyobuni mradi huo, alielezea kufurahishwa kwake na mwanzo mzuri wa kuanza kwa safari mafanikio katika utendaji wa Elimu kupitia Mradi wa Suluhisho la Ubunifu wa Elimu ya Kidijiti (IDES).

Viongozi wa Tume na TEHAMA wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi, Profesa Leonard Mselle (kulia) na Mkurugenzi Mkuu, Dkt. Nkundwe Mwasaga (wa tatu kutoka kulia) walifurahia jambo baada ya kushuhudia maonesho ya kisayansi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Manushi, wilayani Moshi hivi karibuni wakati wa uzinduzi wa maabara ya kisasa ya TEHAMA. Wa pili kulia na Mkuu wa Shule ya SekondarI Manushi, Hamisi Mbawa


“Elimu ndio msingi wa maendeleo, na katika nyakati hizi za kisasa za kidijitali, ni muhimu kutumia Teknolojia ili kukuza mazingira ya kujifunza.

Ubunifu huu utabadilisha mifumo yetu ya elimu kama vile kuwa na darasa la Kompyuta la kisasa lenye uwezo wa kuingia wanafunzi 40 kwa wakati mmoja, Mfumo wa Kusimamia Masomo, Uundaji wa Maudhui, Maktaba za Kidijiti, Ukuzaji wa Ujuzi na Uthibitishaji.

“Katika dunia inayozidi kuwa ya utandawazi, mipaka ya elimu inapanuka. Kupitia Darasa la Mtandao, wanafunzi wanaweza kutumia nyenzo zao za kujifunzia kwa wakati halisi kutoka mahali popote.

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt Nkundwe Mwasaga akikata upete kuashiria uzinduzi wa maabara ya kisasa ya TEHAMA katika Shule ya Sekondari Manushi, wilayani Moshi, Kilimanjaro hivi karibuni. Shule hiyo ya Kata imeweka historia ya kuwa na maabara ya kisasa huku Tume ya TEHAMA ikiahidi kulenga kushawishi wadau wa elimu ili kuzifikia shule nyingine za aina hiyo zaidi ya 4,000 nchini.

Mbinu hii bunifu haileti tu mitindo mbalimbali ya kujifunza, bali pia hujumuisha vipengele shirikishi vinavyoboresha ushiriki wa wanafunzi,” alisema Bahanza.

Aliongeza kuwa, katika soko la kisasa la ajira, ujuzi ni muhimu zaidi kuliko hapo awali, hivyo kusisitiza anaamini ubunifu wa darasa hilo la kisasa utatoa program zinazolenga ujuzi wa vitendo na uidhinishaji zinazotambuliwa na tasnia ya TEHAMA.